Habari

Picha: Wamachinga wa pembezoni mwa Machiga Complex wapoteza mitaji baada ya mabanda yao kubomolewa

Wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga jijini Dar es salaam, Tanzania wamekumbwa na taharuki baada ya kufika katika eneo lao la biashara nje ya jengo la Machinga complex na kukuta vibanda vyao vimebomolewa.

Zoezi hilo limefanyika usiku wa kuamkia Jumatatu na kwa hasira wafanyabiashara hao wakachoma moto barabara kwa kutumia matairi na takataka nyingine.

Wafanyabiashara hao wamedai kuwa walipewa siku tatu kuhakikisha wanaondoa bidhaa zao.
Hata hivyo wamedai kuwa waliandika barua ya kuomba kusitishwa kwa zoezi hilo ili wapatiwe vizimba lakini cha kushangaza ni kwamba wamevunjiwa hata bila kupata majibu ya baraua yao.

Pia wamelalamika kupotea kwa bidhaa zao ambazo baadhi yake zimeibiwa na nyingine hawajui zimepelekwa wapi.

Mfanyabiashara wa machinga Complex Yohana William amelalamika kuwa mtaji wake wote umepotea kwani alikuwa ameaminiwa na mali za watu kufanya biashara lakini vunjavunja hii imemharibia biashara yake, na amepoteza kila kitu.

“Vibanda vyetu vimebomolewa, nimebakia hivihivi kama nilivyo unavyoona nina mkopo wa watu, walikuwa wananiamini kwenye kizimba tuko kikundi pamoja sasa tunashangaa…,” mfanyabiashara huyo amesema kwa masikitiko makubwa.

“Sasa tunashangaa rais ameruhusu wafanyabiashara kama sisi wako barabarani, lakini sisi wafanyabiashara wadogo tuliovumilia miaka yote, miaka sita tuko hapa, hili jengo linaitwa machinga complex sasa tumekuja wamachinga wenyewe tunatolewa. Na pale ambapo wananambia niende sijaelekezwa,” amesema William.

Wakinamama wajasiriamali katika soko hilo walilaumu zoezi hilo la kubomoa vibanda vyao vya biashara ambavyo ndio vilikuwa vinawapatia riziki zao.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents