HabariSiasa

Rais Uhuru Kenyatta alivyokana tuhuma za kutaka kumuua Ruto

Wakati zikiwa zimesalia siku nane kabla ya Wakenya kufanya Uchaguzi Mkuu, Agosti 9, 2022, vita ya kurushiana maneno kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto vimezidi kushika kasi.

Jana Jumapili Julai 31, 2022 Rais Kenyatta amekanusha madai ya kupanga kumuua Ruto huku akimtaka afanye siasa zake pasi na kumhusisha wala kuwadanganya Wakenya.

Akizungumza katika ufunguzi wa barabara ‘Nairobi Expressway’, Kenyatta amesema kwa miaka mitatu Ruto na wenzake wamekuwa wakimtukana na yeye amekaa kimya licha ya kuwa na uwezo wa kuwachukulia hatua.

Rais Kenyatta amesema kujibu matusi na uongo unaonezwa dhidi yake siyo ajenda yake kwa wakati huu anaomalizia kipindi cha utawala wake.

“Haina haja wewe kuwaambia watu kwamba ninataka kukuua. Si umenitusi kwa miaka mitatu na hakuna mtu amekugusa. Si nimekuwa serikalini kwa miaka mitatu na nilikuwa na mamlaka yote?

“Je, wakati huu ambapo ninakaribia kuondoka madarakani na kumkabidhi mtu mwingine atakayechaguliwa ndipo unahisi kwamba ninakuandama?” amehoji Kenyatta.

Rais Kenyatta amesisitiza kuwa hakuna sababu kwa Ruto na wenzake kumtusi kwa sababu yeye amewaonya Wakenya wasikubali kudanganywa hadharani.

“Usiendelee kuwadanganya watu na ninapojibu uwongo wako usiwaambie watu kwamba ninataka kukuua. Wewe uza ajenda yako na porojo nyinginezo na uachane nami. Nitaendelea na kazi yangu hadi nikamilishe. Wewe tafuta kura kutoka kwa wananchi, wakikuchagua sawa, wasipokuchagua basi tutaenda nyumbani pamoja,” Amesema Rais Kenyatta

Hata hivyo akiwa katika kampeni mjini Kapsabet, Kaunti ya Nandi, Ruto amesema haogopi kupambana na Rais Kenyatta na “mradi” wake, Raila Odinga katika sanduku la kura.

“Mradi hautaua watoto wangu, niko tayari kukabiliana nawe katika uchaguzi huu, ukiwa pamoja na mradi wako, huyo mzee wa kitendawili,” amesema Ruto.

“Bwana Rais, umekuwa chanzo cha vitisho nchini Kenya. Usitishe Wakenya. Kazi yako ni kuhakikisha kuwa Wakenya wote wako salama. Acha kutuambia kwamba tutajua wewe ni Rais, vitisho dhidi yangu havitanizuia kuendelea na juhudi zangu za kusaka kura za urais.” amesema Ruto.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents