Habari

Tanzania ina upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi na ganzi: SATA

WAGONJWA wanaopaswa kupewa dawa za usingizi na maumivu hususan wale wanaofanyiwa upasuaji nchini, wapo katika hatari ya kosa huduma hiyo kwa ubora kutokana na upungufu wa wataalamu wa kutoa dawa za usingizi na ganzi.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa kutoa Dawa za Usingizi na Maumivu (SATA), Dk. Edwin Lugazia wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa nne wa chama hicho uliokuwa unajadili mambo mbalimbali yahusuyo fani hiyo pamoja na changamoto zake.

Dk. Lugazia ambaye ni daktari bingwa wa dawa za usingizi na ganzi aliyebobea kwenye upasuaji wa moyo amesema  licha ya Serikali kuweka miundombinu ya kutosha katika sekta hiyo bado kuna chagamoto hiyo ya upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi pamoja na ganzi.

“Katika kutoa huduma hii ya usingizi na ganzi serikali kuanzia ya awamo ya tano na sita zimejitahidi kuweka miundombinu ya kutosha ya kutolea usingizi salama ikiwemo mashine za kutosha, vitendea kazi pamoja na dawa lakini changamoto tuliyonayo ni kutokuwa na watoa huduma wa kutosha wenye weledi”amesema

Amesema katika kukabilina na chagamoto hiyo wamekuwa wakiendelea kutengeneza na kufundisha watalamu watakaoweza kutoa huduma salama za usingizi na ganzi pamoja na kuwahudumia wagonjwa mahututi  wanaohitaji dawa za usingizi.

Aidha amesema mkutano huo umekuwa ulifanyika kila mwaka kwa Wanataaluma kwa lengo la kujadiliana na kubadilisha uzoefu sambamba na mafunzo tofauti tofauti pamoja na kujengeana uwezo katika ngazi ya chini mpaka ya juu hadi ya kimataifa na kuongeza kuwa kupitia mkutano huo watajadiliana chagamoto wanazokubana nazo pamoja na zile zinazokabili Taifa katika huduma za kutoa dawa za usingizi na wagonjwa mahututi.

“Kwa sasa vituo vingi vimeongezwa tunahitaji kukimbizana kutengeneza na kufundisha watoa huduma ambao wataweza kutoa huduma hizi kila mahali . kupitia mkutano huu ambao unafanyika kwa siku mbili na umejumuisha washiriki 250 tutaweza kujengana uwezo, kujadiliana changamoto na kutafuta mbinu mbadala za kukabiliana nazo,” amesema

Kwa upande wake Katibu wa SATA, Dk. John Kweyamba amesema madaktari bingwa ambao wamekuwa wakiingia katika Chama hicho wamekuwa wakipata fursa mbalimbali za kwena kujiendeleza kwenye nchi 83 ambazo jwanahusiana nao hivyo nchi kupata wataalamu waliobobea zaidi na chama kuongeza idadi ya wabobezi katika sekta hiyo.

“Tunakili kuwa changamoto zipo lakini zinaendelea kutatuliwa tunaona zoezi la madaktari wa Samia wanakwenda mikoani na kuwajengea uwezo wataalamu waliopo huko hivyo niwaombe wataalamu wenzangu tuendelee kuwa wamoja na kulijenga taifa letu hasa katika kutoa na kujenga afya bora za wananchi,” amesema Dk. Kweyamba

 

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents