Habari

TMA yatangaza mvua kubwa zitakazodumu kwa siku tano katika mikoa 9 Tanzania

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza mvua kubwa katika mikoa sita bara na baadhi ya maeneo visiwa vya Unguja na Pemba zitakazodumu kwa siku tano kuanzia leo Jumamosi Desemba 28, 2019.

Akitoa taarifa kwa umma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Wilberforce Kikwasi amesema mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa jijini Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, mikoa ya kusini pamoja na Unguja na Pemba ni za siku tano mfululizo kuanzia na kuwataka wananchi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari.

“TMA inatoa tahadhari juu ya uwepo vipindi vifupi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo yaliyopo Kusini mwa nchi yetu hususani Ruvuma, Lindi, Mtwara eneo la kusini mkoa wa Morogoro, mkoa wa Pwani, Dar es Salaam pamoja na maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba.”

“Hali hii ya mvua inatokana na kuendelea kuimarika kwa ukanda wa mvua katika maeneo ya Kusini mwa nchi yetu na hivyo kusababisha kujengeka kwa mawingu makubwa na mazito yanayosababisha mvua kubwa zitakazoambatana na upepo mkubwa na radi hivyo wananchi waliopo maeneo hayo wanatakiwa kuchukua tahadhari,” amesema Kikwasi.

Kikwasi amesema TMA inaendelea kufuatilia kwa karibu maeneo hayo na kutoa mrejesho pale itakapohitajika.

“Taarifa hii inaanza leo Desemba 28, 2019 na ni kwa siku tano zijazo, TMA itaendelea kufuatilia na kutoa mrejesho kupitia miundombinu mbalimbali ya mawasiliano kupitia vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii, televisheni na redio,” amesema Kikwasi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents