Habari

TRA yataifisha Boksi 41 za Mvinyo zenye thamani ya Tsh. Milioni 3

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata na kutaifisha boksi 41 za mvinyo na pombe kali zenye thamani ya Tsh. Milioni 3 zilizokutwa katika duka la jumla jijini Dodoma zikiwa hazina Stempu za Kodi.

Mali hizo za Anthony George, zimekamatwa na kutaifishwa leo wakati Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere akikagua matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs).

Akizungumza mara baada ya kutaifisha boksi hizo, Kichere amesema kuwa, ni wajibu wa muuzaji kuhakikisha kwamba, vinjwaji vinavyostahili kuwekewa Stempu za Kodi vinakuwa na stempu hizo ili kuisaidia Mamlaka kutoza kodi stahiki.

“Inatakiwa stempu za kodi ziwekwe kwenye mzigo kabla mzigo huo haujanunuliwa na wauzaji wa rejareja. Hii itaisaidia TRA kukusanya kodi halali na hatimaye kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali,” alisema Kichere.

Mvinyo na pombe kali zilizokamatwa na kutaifishwa ni pamoja na boksi 27 za Robertson, boksi saba za Jameson, boksi tano za Drostdy Hof na boksi mbili za Alko Dompo.

Aidha, Kamishna Mkuu Kichere ametoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kutoa risiti kila wanapofanya mauzo na wananchi kuhakikisha wanadai risiti kila wanapofanya manunuzi mbalimbali.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents