Habari

Viashiria vitano vinavyokuonyesha kwamba hutakiwi kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi

Je kweli uko tayari kuingia kwenye mahusiano? Kama utajikuta unaangukia kwenye mojawapo ya vitu vitakavyotajwa hapo chini, inamaanisha kuna kazi ya ziada inatakiwa ifanyike kwako ili uwe na mahusino yenye afya au mahusiano yenye malengo na yatakayodumu muda mrefu.

black-woman-beautiful-woman-pretty-photo

Kama unajiona huvutii
Hii inawahusu hasa wanawake au dada zetu. Wao hupenda kuangalia mwonekano wa nje na kufikiri kwamba ukiingia kwenye mahusiano unafikiri mtu mwingine atakwambia wewe ni mzuri au una mvuto, hapo unakuwa umekosea. Ukweli ni kwamba hakuna mtu atakayekuambia wewe ni mzuri kama wewe mwenyewe hujitambui na kama hujiamini. Wewe ni mtu wa thamani na hakuna atakayeweza kufanana na wewe kwasababu uko peke yako. Unapoingia kwenye mahusiano uwe mtu ambaye unatambua wewe ni nani na thamani yako iko wapi. Ukitegemea watu wengine wakuthaminishe, watakuweka kwenye mazingira mabaya au kukuharibu kwa kukulazimisha ufanye wanavyotaka wao au uonekane wanavyotaka wao hivyo unajikuta unapoteza utu wako na hata kuharibu mwili wako.

Kama wewe ni mtu wa visasi na husamehi watu wengine
Huwa unasema umemsamehe mtu lakini hiyo ni ya mdomoni tu, moyoni bado unapanga namna yakuja kulipiza kisasi. Umekuwa unafikiria vitu vilivyotokea miaka ya nyuma na ndio sababu hata sasa kuna watu bado una vinyongo nao. Hii pia inaweka kasoro kwenye mahusiano yako na mpenzi wako wa sasa. Utajikuta mambo mengi unavyochukulia unakumbuka watu wa nyuma walichokufanyia. Inachokubidi kufanya ni kuruhusu kinyongo kiondoke na uponye moyo wako kwa kwenda hatua nyingine bora zaidi.

Wewe ni mtu usiyetaka kubadilika
Kila wakati unasema utafanya vizuri lakini haufanyi chochote, iwe kwenye taaluma yako au biashara na hata imani. Unajua kabisa una mapungufu fulani ambayo unatakiwa kuyafanyia kazi lakini hauyafanyii kazi na mambo yanapotokea unatafuta mtu wa kumlaumu. Kila siku lazima uchukue muda wa kushughulikia tabia zako, hulka na kujitambua vizuri ili uwe mtu wa kuambukiza matendo kwa watu wengine, kuna tatizo kwako mwenyewe.

Huwa huchagui wanaume wa kwenda nao
Kwa kifupi unaweza ukaitwa jalala au hauna mwelekeo ni kama hujui nini unataka. Umekuwa ni mtu ambaye marafiki zako wanakuuliza kwanini uko na mtu huyu au huoni kwamba huyu mtu ana matatizo au ana hiki na hiki na wewe huna majibu? Hapa sizungumzii wale wenye wivu bali nazungumzia kwa wale ambao wanajua umeingia mikono ambayo sio salama na wala hakuna malengo ya maisha ya baadaye hapo. Kumbuka watu wengi wanaweza kuonekana wanakuzungumzia sana kuhusu mtu uliyenae ni kwa sababu ya viwango vyako ulivyosema vinatofautiana na unachokifanya au maamuzi unayochukua sasa. Ni wakati wa kujichunguza mwenyewe na kujua unatakiwa kuwa wapi na nani na kwasababu gani, usifanye mambo bora liende au kufuata mkumbo. Maisha ni mafupi sana hivyo, hivyo fanya maamuzi sahihi ambayo yatakusaidia kuishi kila siku ukiwa na furaha na amani.

Hauna furaha
Kama hauna furaha sasa hivi, kwanini unaruhusu kuingia kwenye mahusiano mtu ambaye aje kushughulikia matatizo yako ya kutokuwa na furaha? Hakuna mtu ambaye anataka kuingia kwenye mahusiano na mtu ambaye ni mzigo kimawazo au kihisia, lazima mahusiano hayo yatakuwa na matatizo kwani wewe furaha yako itategemea sana yule mwenzako hivyo unakuwa unamnyonya kihisia. Ingia kwenye mahusiano ukiwa na furaha au hisia zako ziko sawasawa inamaanisha kwamba uko vizuri kiasi kwamba usiwe mzigo upende wa pili, kila dakika umenuna, una mawazo n.k. Fanya upendo wako hakikisha unatafuta furaha kabla ya kuingia kwenye mahusiano, hivyo badilisha mtizamo wako na ufanye mambo yenye akili. Kumbuka tuko kwenye jamii ambayo wakati wote huwa hatupendi kuonekana tuna tatizo fulani, ila kuna matatizo makubwa ndio maana mambo mengi hayaendi kama yalivyokusudiwa.

Ninajua unajua mambo mengi hivyo nimetoa kidogo kuweza kusaidia pale ambapo pamepungua. Jambo la msingi ni kuwa ufahamu wako ukikua na kubadilika unaweza kubadilisha hali ya mambo yanavyokwenda na kuwa bora zaidi. Majibu yote ninaamini uko nayo ni suala tu la kuyafanyia kazi.

Awali Mwaisanila

A Personal Career Development specialist, passionate about empowering emerging generations of student, graduates and working class.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents