Habari

Video: Wazazi toeni ushirikiano kesi za ukatili kwa watoto – Dkt Jingu

Baadhi ya Wazazi na walezi Mkoani Rukwa wameelezwa kuchangia kuchelewesha upatikanaji wa haki kwa waathirika wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwa kushindwa kutoa au kuwazui watoto kutoa ushaidi mahakamani.
Akizungumza na wadau wa Jukwaa la Haki Jinai Mkoani hapa, Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewataka Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuhakikisha jamii inabadili mitazamo na kushiriki katika mchakato wa kupatikana haki kwenye kesi za ukatili kwa watoto.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa Maafisa Ustawi na Maendeleo wa Jamii wana jukumu la kubadili fikra za jamii ione umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya Serikali katika kushughulikia mashauri ya Ukatili dhidi ya watoto na kwamba masuala haya ni makubwa na yanaacha makovu makubwa kwa watoto.
Amesema Jamii ikiacha matendo hayo yaendelee bila kutoa adhabu, yakiachwa na kutoa adhabu Watoto watakuwa wanaumia na hatimaye kusababisha madhara kwa Taifa zima.
“Niwaambie tu maumivu ya kufanyiwa ukatili kwa watoto yasipotibiwa yanasababisha madhara makubwa kwa watoto wenyewe na jamii”alisema Dkt. Jingu
Dkt. Jingu pia ameiasa Jamii kuwa mstari wa mbele katika kuwarekebisha watoto wanaokinzana na Sheria kuanzia ngazi ya familia na wadau wote muhimu , ikiwemo kuzuia vitendo visivyofaa.
Amesisitiza pia kuwatunza watoto na kuacha mfumo wa sasa wa kuwaacha watoto kulelewa na wasaidizi wa nyumbani pamoja na televisheni, hali inayochangia mmomonyoko wa maadili.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome, akizungumza katika kikao hicho amewataka watendaji wote wanaohusika katika mchakato wa utoaji haki, kufuata Sheria, kanuni na taratibu na kufanya kazi kwa weledi ili wananchi wapate haki kwa wakati.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora Dkt. Laurean Ndumbaro ameahidi kuziba pengo la uhaba wa watumishi hasa wanasheria katika Wilaya ya Sumbawanga na Magereza ya Namanyere Nkasi ili iweze kufanya kazi.
Awali akiwasilisha taarifa ya Hali ya utoaji Haki katika Mkoa huo, Mwanasheria wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Frida Hava alisema ushirikiano wa Idara mbalimbali katika utoaji haki umeleta mafanikio chanya kwa ustawi wa wananchi wa Mkoa huo.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Mpango wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Faustina Vallery amesema changamoto zilizopo ni pamoja na kukosa mahabusu za watoto pamoja na uhaba wa watumishi japokuwa wanapata ushirikiano na mamlaka nyingine Mkoani hapo.
Ziara ya Makatibu Wakuu hao inafanyika kwa lengo la kujadili na watendaji na kuona namna ya kutatua changamoto za masuala yanayozigusa Wizara hizo kwa pamoja hususani suala la kushughulikia mfumo wa haki za makosa ya jinai kama ya ukatili dhidi ya watoto.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents