Habari

Viongozi wakuu wa dini kukutana leo

Viongozi wakuu 20 wa dini nchini, wanatarajia kukutana leo jijini Dar es Salaam kujadili athari za ndoa za utotoni kwa maendeleo ya watoto, familia na taifa kwa ujumla.

Na Ananilea Nkya, TAMWA

 

Viongozi wakuu 20 wa dini nchini, wanatarajia kukutana leo jijini Dar es Salaam kujadili athari za ndoa za utotoni kwa maendeleo ya watoto, familia na taifa kwa ujumla.

 

Viongozi hao pia watazungumzia vikwazo vilivyopo katika kukabiliana na ndoa za utotoni na nini serikali, madhehebu ya dini na wananchi wanaweza kufanya ili kuepusha watoto wa kike kuolewa wakiwa na umri mdogo.

 

Mkutano huo umeandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Nchini (TAMWA) ikiwa ni sehemu ya mipango yake ya kuelimisha na kuhamasisha umma ili wadau mbalimbali wachukue hatua sahihi kuondoa tatizo hilo.

 

Miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni Sheikh Mkuu, Mufti Issa Shaaban Simba na
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Nchini, Sheikh Mussa Undecha.

 

Wengine ni Mkuu wa Kanisa Katoliki Nchini, Mhadhama Kardinali Polycarp Pengo na Mkuu wa Kanisa la Kilutheri nchini (KKKT) Askofu Alex Malasusa.

 

TAMWA imeandaa mkutano huo kwa kutambua umuhimu wa viongozi wa dini katika kujenga na kutunza maadili mema ya jamii na kuhimiza maendeleo ya watu na taifa.

 

Aidha, TAMWA inatambua kuwa ndoa za utotoni zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kukwamisha mipango ya serikali ya kuwaendeleza watoto wa kike kielimu ili watakapokuwa watu wazima waweze kutekeleza kikamilifu majukumu yao kwa familia, jamii na taifa.

 

Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa vifo 24 vinavyotokana na uzazi vinatokea kila siku hapa nchini na waathirika wengi ni wale wa ndoa za utotoni.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents