Habari

Vurugu zaibuka Msikitini

Waumini 10 wa Msikiti mpya wa Masjid Badri uliopo Mtoni Mtongani, jijini Dar es Salaam, wamejeruhiwa kwa mawe baada ya kuibuka vurugu kubwa kati ya uongozi wa zamani wa wazee na vijana wa Msikiti huo.

Na Romana Mallya

 
Waumini 10 wa Msikiti mpya wa Masjid Badri uliopo Mtoni Mtongani, jijini Dar es Salaam, wamejeruhiwa kwa mawe baada ya kuibuka vurugu kubwa kati ya uongozi wa zamani wa wazee na vijana wa Msikiti huo.

 

Vurugu hizo ziliibuka baada ya Sala ya Adhuhuri iliyofanyika msikitini hapo.

 

Chanzo cha waumini hao kuanza kurushiana mawe ni baada ya watu wasiofahamika kufuta jina la Msikiti na kuandika jina jipya la `Masjid Na-Hija`.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Bw. Emmanuel Kandihabi alisema chanzo cha vurugu hizo kinadaiwa kuwa ni uongozi wa wazee kukaa kwa muda mrefu madarakani bila kufanya uchaguzi.

 

Alisema uongozi huo ambao hata hivyo hakuutaja unaongozwa na nani, umekaa madarakani kwa kipindi cha miaka saba mfululizo.

 

Alisema hali hiyo ndiyo iliyochangia kuwepo kwa mvutano kati ya pande za uongozi huo na vijana wa Msikiti huo.

 

Kamanda Kandihabi alisema baadaye pande hizo zilikubaliana uchaguzi mpya ufanyike baada ya Iddi el Fitri.

 

Alisema wakiwa katika mipango hiyo, juzi baada ya sala hiyo, ndipo watu ambao hawajafahamika walibadili jina la Msikiti huo kwa kutumia rangi.

 

Alisema baada ya jina hilo kubadilishwa na watu hao, ndipo ushindani kati ya vijana na uongozi wa wazee ulipoanza na hatimaye kuanza kurushiana mawe wenyewe kwa wenyewe.

 

`Baada ya uongozi wa wazee kuwahoji vijana na kushindwa kuafikiana, ndipo walipoamua kurushiana mawe ambayo yaliwajeruhi waumini 10,` alisema.

 

Kamanda Kandihabi aliwataja majeruhi hao kuwa ni Iddi Bilingi (70), Ramadhani Hussen (55), Issa Hussen Mwakilinga (45) na Hussein Ramadhan (18) ambao kwa pamoja walijeruhiwa miguuni.

 

Wengine ni Athuman Maputi (25), Mikidadi Amri (45), Iddi Hussein (55) ambao waliumia sehemu za kichwani wakati Hashim Ramadhani (20), Mlinga Nassor (26) na Seleman Juma (33), haijafahamika walipata majeraha sehemu gani za miili.

 

Kamanda Kandihabi alisema majeruhi wote walitibiwa katika hospitali ya Temeke na kuruhusiwa hali zao zinaendelea vizuri.

 

Alisema juhudi za kuwasaka waliosababisha vurugu hizo zinaendelea na kwamba mpaka sasa hakuna anayeshikiliwa.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents