Habari

Waliokatika misuli, mishipa kutokana na ajali wafanyiwa upasuaji rekebishi

WALIOKATIKA MISULI NA MISHIPA KUTOKANA NA AJALI WAFANYIWA UPASUAJI REKEBISHI MUHIMBILI.

Hospitali ya Taifa Muhimbili imewafanyia upasuaji rekebishi wagonjwa 23 waliopata ajali na kukatika baadhi ya misuli pamoja na mishipa ya fahamu katika sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo mikono na miguu.

Kambi hiyo ilianza tarahe 20 hadi 28 Novemba, 2023 ambapo imehusisha Madaktari Bingwa wa Upasuaji MNH kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Taasisi ya Rafiki ya nchini Australia .

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo, Mkuu wa Kitengo cha upasuaji rekebishi Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Laurean Rwanyuma amesema kambi hiyo imefanyika kwa mafanikio makubwa ambapo wamefanikiwa kuunganisha mishipa na misuli ya wagonjwa ambao walipata ajali iliyosababisha viungo hivyo kuumia.

“Mtu akipata ajali anaweza kukatika mikono au miguu na kusababisha baadhi ya mishipa ya fahamu kukata mawasiliano hivyo tunachokifanya nikuunganisha mishipa hiyo kwa kuchukua mishipa ya fahamu kutoka sehemu nyingine hasa sehemu ya mguu na kuiunganisha katika sehemu iliyopoteza mawasiliano katika mwili ili iweze kurejea katika hali yake ya awali”amefafanua Dkt. Rwanyuma

“Pamoja na kuwafanyia upasuaji wagonjwa waliopata ajali mbalimbali pia tumewafanyia wagonjwa wengine ambao walikuwa na uvimbe wenye saratani katika sehemu ya kichwa hivyo tumeondoa uvimbe huo na kufanya marekebisho katika sehemu hiyo” amesema Dkt. Rwanyuma.

Dkt. Rwanyuma ameongeza kuwa kabi hiyo imeenda sambamba na kutoa mafunzo kwa wataalam wa mazoezi tiba ili kuweza kuwahudumia wagonjwa hao mara wanapoanza kuja kliniki baada ya kufanyiwa upasuaji huo.

Kwa Upande wake Daktari Bingwa wa Usingizi na Mshauri wa Upasuaji kutoka Taasisi ya Rafiki amewapongeza wataalam wa Muhimbili kwa ushirikiano waliounesha katika kambi hiyo na kuseme kuwa watafanya kambi nyingine kama hiyo mwakani mwezi wa tatu.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Julieth Magandi ameishukuru taasisi hiyo kwa kushirikiana na Muhimbili na kuwaomba ushirikiano huo uendelee kwa kuwa una manufaa makubwa katika kuboresha huduma za upasuaji Muhimbili.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents