Habari

Wanaowakashifu na kuwakejeli viongozi kumulikwa

TUME YA HAKI ZA BINADAMU WATAKIWA KUWAMULIKA WANAOWAKASHIFU NA KUWAKEJELI VIONGOZI

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kujipambanua katika majukumu yao na kutambua kazi inayofanywa na Serikali katika kutetea Haki za Binadamu na kuangazia baadhi ya watu wanaovuruga na kukashifu haki za wengine wakiwemo Viongozi kwa sababu ya uwepo wa uhuru wa kujieleza.

Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo katika makao makuu ya Tume Kilimani jijini Dodoma ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kuzitembelea Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kujifunza na kufahamu majukumu yao katika kufanikisha kazi za Wizara.

“Jukumu la Tume ni kuangalia kwa kiwango gani haki za Binadamu na Utawala Bora zinatekelezwa na Taasisi mbalimbali za Umma au hata watu binafsi katika majukumu yao.Yapo mambo mengi ambayo Serikali imefanya yanayogusa haki za Binadamu lakini je katika ripoti zinazoandikwa na Tume hayo wameripotiwa?” Alisema Sagini

Aliendelea kusema, “Serikali ya. Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya maamuzi magumu kufanya elimu ya msingi kuwa miaka kumi, utoaji wa elimu bila malipo mpaka kidato cha sita, ujenzi wa Zahanati na Hospitali katika maeneo mbalimbali, kwenye Demokrasia imetoa uhuru wa watu kutekeleza majukumu yao ya kisiasa yote haya yanalenga kulinda Haki za Binadamu.

Lakini wanaibuka watu na lugha za kejeli,lugha za matusi na lugha za kufedhehesha Viongozi wetu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iangalie na kujitokeza hadharani na kuelimisha watu juu ya yale wanayoyaona na yale yanayotendwa na Watanzania.”Alisema Naibu Waziri.

Aidha, Sagini ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuboresha mahusiano na ushirikiano mahali pa kazi ili kuleta mafanikio na ufanisi katika kutimiza malengo ya Taasisi.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents