Habari

Wasio kunywa maji mengi hatarini kupata athari hizi kubwa kiafya, Daktari bingwa azitaja

Watu wanaokunywa maji kidogo kulinganisha na kiwango cha chumvi kinachotengenezwa mwilini, wako hatarini kupata mawe kwenye figo na mfumo wa mkojo kwa ujumla, imeelezwa.

Daktari Bingwa wa Mfumo wa Mkojo na Upandikizaji wa Figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk. Remigius Rugakingira, aliyasema hayo alipotoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari wakati wa ziara ya timu ya maofisa habari wa wizara na taasisi zake mkoani Dodoma jana.

Dk. Rugakingira alisema hospitali hiyo tangu kuanzishwa kwake imepokea wagonjwa wengi wenye mawe kwenye mfumo huo, akibainisha kuwa tatizo hilo linawakumba watu wa rika zote.

Alisema awali walikuwa wanapokea wastani wa wagonjwa watano kwa mwezi, lakini kwa sasa si chini ya 32 kwa mwezi, wakitoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Kama unakunywa maji kidogo kulinganisha na aina ya chumvi inayotengenezwa mwilini, una hatari ya kupata mawe, pia kuwa na bakteria wengi katika mfumo wa mkojo, unaweza tengeneza mawe,” alisema.

Alibainisha kuwa tatizo hilo ni kwa wanaume na wanawake, lakini linategemea na mhusika anakunywa maji kiasi gani na mkojo unatoka kiasi gani.

“’Nature’ ya mawe ambayo tunayaona ni magumu na tuna historia hapa tulitoa jiwe lenye sentimita 4.5 ambalo tumetoa kwenye kibofu, na sentimita 2.6 ambalo limetolewa kwenye figo ,” alisema.

“Tumeweza kufanyia upasuaji mtoto wa miaka minne alikuwa ana jiwe kubwa kwenye njia ya mkojo, leo (jana) nimemtoa mtu mwenye umri wa miaka 96, alikuwa na jiwe kwenye njia ya mkojo,” alisema.

Daktari huyo alisema mashine ya kusaga mawe hayo itafungwa mwezi ujao kwenye hospitali hiyo na itakuwa ya kisasa na mfumo mzima umegharimu takriban Sh. bilioni sita.

“Uwekezaji wa mashine hii ni mkubwa na wa kisasa, ni sawa na Ujerumani na nchi zinginge, itatumia mionzi, mfumo utakuwa unatumia kamera, unaenda kwenye eneo la jiwe na kulivunja, na njia nyingine ya pili ni kutumia mfumo wa kufungua,” alisema.

Alisema kuna wagonjwa kutoka nchi za Comoro, Saudi Arabia, Ghana na Uganda wamefanyiwa upasuaji wa kuondoa mawe.

Alipoulizwa kuhusu gharama, daktari huyo alisema gharama ya kutibu tatizo hilo ni kubwa, lakini katika hospitali hiyo gharama yake inahimilika.

“Tunasita sana kuzungumzia suala la gharama maana mtu unamwambia Sh. milioni moja au mbili anaona ‘eeh Mungu wangu, naenda kufa!’, wakati ukipiga gharama za nje ya nchi ni kubwa,” alisema.

Mtaalam huyo alisema mtu ambaye jiwe limesagwa, ataruhusiwa siku hiyo hiyo, lakini aliyefanyiwa upasuaji, atakaa hospitali kwa kipindi cha kuanzia wiki moja hadi mbili.

“Wengi wanaokuja hapa wanaotibiwa UTI, mtu anasema nimetibiwa UTI, nimepewa antibiotic nyingi, cha kwanza jiwe linapokuwapo pale, linavutia bakteria, hao bakteria watasababisha uharibifu.

“Kuna wengine wanakuja wanasema wanatokwa na damu kwenye njia ya mkojo, sasa pale ni kitu kingine, lakini likikaa sana, likaharibu seli zikawa zinaota kwenye mpangilio ambao siyo sahihi, inaweza kusababisha kansa,” alisema.

Daktari bingwa huyo alitoa wito kwa watanzania kujenga utamaduni wa kufanya vipimo vya afya mara kwa mara ili kupata matibabu.

Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Kessy Shija, alisema madhara ya mawe ni pamoja na kuziba njia ya mkojo na ndani ya figo yanaharibu seli.

“Madhara yapo kama hayo na matokeo yake kile kiungo kinakufa kama hutafanya matibabu yake,” alisema.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents