Habari

Watu zaidi ya 400 wakosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kujaa maji Ifakara

Watu zaidi ya 400 wanaoshi Kata za Viwanja Sitini, Kibaoni, Mbasa na Katindiuka, Halmashauri ya Ifakara Mji wilayani Kilombero, mkoani Morogoro wamekosa makazi baada ya nyumba zao kujaa maji na nyingine kubomoka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Dustan Kyobya na kueleza kuwa mafuriko yaliyotokea kwa mara nyingine yamesababishwa na kujaa kwa Mto Lumemo na kumwaga maji kwenye makazi ya watu.

Amesema watu hao kwa sasa wamepelekwa shule ya Msingi Ifakara ambako watakuwepo kwa muda, huku wakipatiwa msaada na serikali na kwamba mafuriko hayo pia yameathiri shughuli za kibiashara.

“Maji yameingia kwenye baadhi ya nyumba za watu, maduka na kuharibu mali na bidhaa mbalimbali, “ amesema Kyobya.

Pia amesema majengo ya umma nayo yamezingirwa na maji ikiwemo Shule ya Sekondari ya Kashungu na Kituo cha Afya Mbasa na kuharibu barabara kwenda katika kituo hicho.

“Kwa sasa Serikali tunaendelea na uokoaji kwa kuwa bado mvua zinanyesha na hatujui maji yatapungua baada ya muda gani, “ amesema Kyobya.

Naye Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilaya ya Kilombero, Haji Madulika amesema wanatumia Boti iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), ili kuwaokoa wananchi kwa kushirikiana na vijana wa skauti, ambapo kazi hiyo itaendelea hadi pale maji yatakapopungua.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi hilo mkoa wa Morogoro, Shabani Maruguja amesema wameweka kambi ya muda mjini Ifakara kutokana na kata zaidi ya sita zimekuwa zikikumbwa na mafuriko mara kwa mara kuleta athari kwa wananchi na mali zao na kwamba watu zaidi ya 50 ambao nyumba zao ziliingiliwa na maji wameshatolewa.

“ Tupo Ifakara na tumeweka kambi ya muda kwa ajili ya kutoa msaada wa uokoaji baada ya mafuriko kutokea tena na kata zilizoathirika zaidi ni Mbasa na Katindiuka, ambapo watu 50 mpaka sasa wameokolewa, “ amesema Maruguja.

written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents