Habari

Wizara ya afya yazindua mfumo wa TEHAMA kwa vituo vya kutolea huduma

Wizara wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua mfumo mpya wa TEHAMA kwa vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa na lengo la kuboresha utoaji wa huduma za afya katika vituo vyote hapa nchini.

Uzinduzi huo umefanywa na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile leo, Jijini Dodoma ambapo amesema ana uhakika usajili wa vituo vya afya utaenda haraka.

“Nina uhakika maombi ya usajili wa vituo vya afya sasa yataenda kwa haraka. Waombaji watajaza fomu na kulipia hukohuko walipo bila kufika ofisini na vile vile watakuwa na uwezo wa kutumia mfumo kwa kutumia simu zao,” alisema Dkt. Ndugulile.

Amesema Sekta ya Afya ni miongoni mwa sekta muhimu katika Serikali ya Awamu ya Tano ambapo sekta hiyo ni ya tatu kwa kupata bajeti kubwa. Aidha kwa mwaka huu wa fedha jumla ya vituo vya afya 208 vimeboreshwa kwa ajili ya kutoa huduma ya dharura ya mama na mtoto.

Dkt. Ndugulile amesema ndani ya bajeti hii vituo vya afya 67 vitajengwa nchini pamoja na hospitali za rufaa kwa mikoa ambayo haina hospitali za rufaa.

Wakati huo huo, Waziri Ndugulile ameutaka Mfuko wa Taifa wa Bima wa Afya (NHIF) kufanya majukumu iliyopewa ikiwa ni pamoja kusajili vituo vyenye uwezo wa kutoa huduma kutokana na vigezo vilivyowekwa na mfuko huo na kuziachia mamlaka nyingine majukumu yake ya kukagua vituo hivyo kama vile mikataba ya kazi ya wafanyakazi wa vituo husika.

Aidha ameutaka mfuko huo kutafakari juu ya masharti yaliyowekwa katika kusajili vituo ambapo kituo hakiwezi kusajiliwa mpaka kiwe katika uangalizi na mfuko huo kwa miaka isiyopungua mitano.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Otilia Gowele amesema kanuni mpya za sheria ya uongozi wa hospitali za watu binafsi zitasaidia kusogeza huduma kwa wananchi pia hospitali hizo kutoa huduma kulingana na mahitaji ya sasa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents