Bongo5 MakalaFahamuHabari

Zaidi ya watu 40 wakutwa wamekufa kwenye lori

Takriban watu 46, wanaoaminika kuwa wahamiaji, wamepatikana wamefariki kwenye lori lililotelekezwa viungani mwa San Antonio, Texas. Afisa wa zima moto alisema watu 16 wakiwemo watoto wanne pia wamepelekwa hospitalini.

San Antonio, ambayo ni 250km (maili 150) kutoka mpaka wa Marekani na Mexico, ni njia kuu ya kupita kwa watu wanaosafirishwa kwa njia haramu.

Charles Hood, Mkuu wa Zimamoto wa San Antonio, alisema wahudumu wa dharura walifika katika eneo la tukio karibu 18:00 ndani (23:00 GMT) baada ya kupata taarifa za mtu aliyefariki.

Maafisa wa zimamoto walipata ‘’trela likiwa na mwili nje na kadhaa ndani na wangeweza kuona ndani wakati milango ilipofunguliwa.

Aliongeza kuwa lori hilo halikuwa na kiyoyozi kinachofanya kazi na kwamba ndani yake hakukuwa na maji.

Kulingana na kituo cha runinga cha KSAT, gari hilo liligunduliwa karibu na njia za reli katika Upande wa Kusini Magharibi mwa San Antonio.

Idadi kubwa ya wahudumu wa dharura, wakiwemo polisi, wazima moto na wahudumu wa gari la wagonjwa, walionekana wakizunguka lori hilo kubwa.

Mkuu wa Polisi wa San Antonio William McManus alisema uchunguzi huo sasa umekabidhiwa kwa serikali kuu na watu watatu wanazuiliwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico, Marcelo Ebrard, alisema balozi mdogo wa nchi hiyo alikuwa njiani kuelekea eneo la ugunduzi huo, lakini akaongeza kuwa mataifa ya wahasiriwa bado hayajajulikana.

Gavana wa chama cha Republican cha Texas Greg Abbott alimlaumu Rais wa Marekani Joe Biden kwa vifo hivyo, akivitaja kama ‘’matokeo ya sera zake mbaya za mpakani’’.

Beto O’Rourke, mgombeaji wa chama cha Democratic anayechuana na Bw Abbott, alisema ripoti hizo ni mbaya na akataka hatua za haraka zichukuliwe kusambaratisha biashara za usafirishaji haramu wa binadamu na badala yake kufungua njia za uhamiaji halali.

Uhamiaji ni suala lenye utata la kisiasa nchini Marekani, ambapo mwaka jana idadi kubwa ya wahamiaji wasio na hati walizuiliwa wakivuka kuingia nchini kutoka Mexico – wengi wakisafiri kwenye njia hatari na zisizo salama.

Hali ya hewa ya San Antonio ni joto katika miezi ya kiangazi na halijoto huko ilifikia 39.4C (103F) siku ya Jumatatu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents