Aina mpya ya madawa ya kulevya yakamatwa

Ni mwezi mmoja tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mbeya kuwaachia huru watuhumiwa 11 wa usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia tumbo la marehemu Kombo Siriri, Jeshi la Polisi Mbeya limekamata aina mpya ya dawa hizo

Madawa


 


Ni mwezi mmoja tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mbeya kuwaachia huru watuhumiwa 11 wa usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia tumbo la marehemu Kombo Siriri, Jeshi la Polisi mkoani humo, limekamata aina mpya ya dawa hizo zikisafirishwa kutoka Kenya kuelekea Afrika Kusini ambazo inasemekana ni hatari zaidi kwa maisha ya binadamu.



Madawa hayo ambayo yanajulikana kwa jina la Rohyponol ambayo kila vidonge 6000 vinadaiwa kuwa na thamani ya hali ya juu kuliko aina yoyote inayofahamika hapa nchini, jambo ambalo linaashiria kuwa wasafirishaji hao wamekubuhu hivyo uangalifu wa kina unatakiwa katika kudhibiti upande wa biashara hiyo.


 


Wakati mwezi uliopita, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, iliwaachia huru watuhumiwa 11 kati ya 13 waliodaiwa kusafirisha madawa yenye thamani ya sh. milioni 23 katika tumbo la marehemu Siriri wakizisafirisha kupitia Zambia kutoka Afrika Kusini.


 


Akizungumzia kukamatwa kwa dawa hizo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Suleiman Kova, alisema aina hiyo ya dawa iliwahi kukamatwa kwa mara ya kwanza huko nchini Marekani mwaka jana na kwamba mtandao huo wa dawa aina hiyo umeanza kuingia tena nchini.


 


Wafanyabishara wawili wakazi wa Nairobi na Mombasa Kenya, aliowataja kwa majina ya Stephen Juma ‘Obula’ au ‘Kalius Abdul’ (32) mfanyabiashara wa Nairobi na Ali Hussein Abood ‘Faraji'(22) mkazi wa Mombasa wanashikiliwa na Polisi kutokana na kusafirisha dawa hizo kinyume cha sheria.


 


Kamanda Kova alisema taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa hao ziliripotiwa na raia wema ambao waliwatilia shaka wafanyabiashara hao na kwamba dawa hizo zilikutwa katika kasha linalotumika kuwekea chakula aina ya Cornflakes, ambapo pia kulikuwa na mbinu za kuzificha kwa kusafirisha katika njia tofauti.


 


Alisema watuhumiwa hao pia walikutwa na gramu 300 za bangi katika vifurushi vinne na kwamba walipofika eneo la ukaguzi wa mizigo makachero wa Polisi waliwatia mbaroni na kuwapekua na kukutwa na aina hiyo ya dawa za kulevya.


 


Alisema aina hiyo ya dawa huleta madhara kwa mtumiaji ambapo kwa mujibu wa taarifa za kidaktari, hutumika kwa ajili ya nusu kaputi na wahalifu hutumia aina hiyo ya dawa kulewesha abiria au kutumia katika kinywaji kwa lengo la kufanya ubakaji na haitoi harufu yoyote wala haina ladha katika kinywaji.


 


“Mtumiaji hawezi kugundua aina hiyo ya dawa kama imewekwa katika kinywaji wala hawezi kujua kwa kuwa haina ladha yoyote, hivyo anaweza kunywa kinywaji na kulewa mara moja,” alisema.


 


Kamanda Kova alisema iwapo mtumiaji atatumia dawa hiyo anaweza kupoteza fahamu kwa zaidi ya saa 24.


 


Wakati huo huo, mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu (TIA) jijini hapa, Nibwene Gregory (30), amelazwa katika hospitali ya Mbeya Surgical akidaiwa kupewa aina hiyo ya dawa za kulevya.


 


Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo juzi, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya binafsi, Dkt. Eliud Mwakalobo, alisema mwanafunzi huyo aliletwa hospitalini hapo akiwa hajitambui na baada ya kumchunguza alibaini kuwa amepewa aina fulani ya kilevi kisicho na harufu.


 


Alisema kwa mujibu wa maelezo ya wasamaria wema waliomleta mgonjwa huyo ni kwamba alitiliwa kitu katika kinywaji alichokunywa na hivyo kumsababishia kupoteza nguvu na fahamu na kutokana na hali ya uzito wa mgonjwa angechelewa kufika hospitalini hapo angeweza kulala kwa zaidi ya saa 24.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents