Habari

Ajinyonga baada ya kupima kwa hiyari

MWANAFUNZI wa kidato cha sita katika shule ya sekondari St. Aggrey jijini hapa amejinyonga kwa kamba ya begi lake baada ya kubaini kuwa ameathirika na UKIMWI.

Na Rashid Mkwinda, Mbeya


MWANAFUNZI wa kidato cha sita katika shule ya sekondari St. Aggrey jijini hapa amejinyonga kwa kamba ya begi lake baada ya kubaini kuwa ameathirika na UKIMWI.


Kijana huyo, Frank Sanga (22), mkazi wa kitongoji cha Uyole katika mtaa wa Mwawanji jijini hapa, anadaiwa kujiua Desemba 10 mwaka huu saa 12 jioni siku chache baada ya kupima kwa hiyari katika kituo cha Ushauri Nasaha.


Akitoa taarifa za tukio hilo jana, kaka wa marehemu ambaye ni mfanyabiashara wa Uyole, Bw.Justin Sanga, alisema aligundua kifo cha mdogo wake alipoingia chumbani mwake na kukuta akiwa ananing’inia katika dari la chumba anamolala.


Alisema baada ya kuona hali hiyo, alimsogelea na kugundua kuwa alikuwa amejinyonga na pia aliuona ujumbe aliouacha ukieleza kuwa ameamua kujinyonga baada ya kupima na kugundulika kuwa ameambukizwa UKIMWI.


Bw.Sanga alisema aliamua kwenda kutoa taarifa za tukio hilo katika kituo cha Polisi Uyole, ambao walifika na kuuchukua mwili na kuupeleka katika hospitali ya rufaa ya Mbeya kwa ajili ya uchunguzi.


Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Bibi Monica Madembwe, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mbeya na kwamba mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi, ndugu wa marehemu wataruhusiwa kuuchukua kwa maziko.


Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mbeya walidai kuwa vifo vya aina hii vinaweza kuepukwa ikiwa watoa ushauri nasaha watakuwa makini kuwapa ushauri wa kutokata tamaa wale wanaobainika kuambukizwa ugonjwa huo.


Akizungumza hivi karibuni katika kilele cha siku ya UKIMWI duniani, Mshauri wa UKIMWI wa Jiji la Mbeya, Dkt. Hebel Luvanda, alisema kitendo cha kujulikana kuwa mtu ameambukizwa UKIMWI baada ya kupima ni hatua ya mwanzo ya kujua namna ya kuishi kwa matumaini.


“Haipaswi kwa mtu aliyejifahamu kuwa ameathirika na ugonjwa huo akakata tamaa ya kuishi na kujitafutia maisha…wapo wanaoishi na virusi kwa zaidi ya miaka 15 na wanaendesha maisha yao na kuziandalia familia zao maisha kabla ya kifo,” alisema Dkt. Luvanda.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents