Habari

Ardhi vita Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), inakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya ardhi yanayofanywa na baadhi ya maofisa na wananchi katika miradi ya wawekezaji kwenye sekta ya utalii Visiwani humu.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima


SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), inakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya ardhi yanayofanywa na baadhi ya maofisa na wananchi katika miradi ya wawekezaji kwenye sekta ya utalii Visiwani humu.


Hali hiyo imesababisha migogoro mikubwa ya ardhi katika vijiji vya Nungwi, Kidoti, Kiwengwa na Matemwe na kuanza kutia dosari kubwa maendeleo ya sekta ya utalii, ambayo hivi sasa inachangia asilimia 25 ya pato visiwani humo.


Uchunguzi uliofanywa na waandishi wetu, umegundua kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa uuzaji wa ardhi unaodaiwa kufanywa na baadhi ya maofisa wa serikali na wananchi ambao wamejigeuza mawakala wa uuzaji ardhi kwa wawekezaji wa kigeni.


Katika Kijiji cha Nungwi, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, familia moja imelalamika kuporwa eneo lao la ardhi kwa njia za ujanja uliofanywa na mwekezaji anayemiliki mradi wa hoteli moja, ambaye anadaiwa kuongeza eneo la ardhi kutoka mita 150 hadi 283.


Hali hiyo imesababisha familia hiyo ya marehemu Ussi Haji, kufungua malalamiko Idara ya Ardhi na Usajili na baadaye likapanda hadi kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji Vitegauchumi.


Kwa mujibu wa barua ya Aprili 16 kutoka kwa wanafamilia hao kwenda kwa meneja wa hoteli hiyo, wametaka walipwe fidia kwa eneo lililochukuliwa bila ya kuwepo kwa makubaliano.


Katika barua hiyo, wananchi hao wametaka kulipwa sh milioni 88.3 kama fidia kutokana na miti aina ya mivinje, vibanda vilivyobomolewa, gharama za kufuatilia suala hilo pamoja na kulipwa eneo la ardhi lililozidi kwa kufuata taratibu za mwanzo za mauziano au kurejeshewa eneo hilo.


Aidha, wananchi hao wametuma nakala ya malalamiko hayo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitegauchumi (ZIPA), Mkurugenzi wa Ardhi na Usajili na Mkurugenzi wa Hoteli na Utalii.


Mwaka 1995, wanafamilia hao waliuza eneo lenye urefu wa mita 150 kwa mwekezaji huyo kwa thamani ya sh milioni 12.


Mkurugenzi wa Idara ya Ardhi na Usajili, Salum Simba, amethibitisha kuwepo malalamiko hayo na kwamba suala hilo hivi sasa linajadiliwa katika ngazi ya mkoa huko Kaskazini Unguja.


“Kilichojitokeza hivi sasa ni wananchi wengi katika maeneo ya utalii kupatwa na tamaa kutokana na maeneo hayo kuuzwa kwa bei ya juu kwa wawekezaji kutoka nje,” alisema.


Alisema kwamba eneo linalolalamikiwa kuongezwa halijapimwa na maofisa wake, lakini hata hivyo hakusema hatua gani zitachukuliwa kutokana na mwekezaji kudaiwa kutanua hoteli bila ya kuzingatia matumizi ya ardhi.


Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, hivi sasa kumeibuka kundi la mawakala wanaochukua ardhi kwa wanavijiji na kuwauzia wawekezaji kufunga mikataba ya kienyeji ambao haishirikishi wanasheria.


Hali hiyo imejitokeza katika vijiji vya Kidoti na Kilimani katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako baadhi ya wananchi wameuza maeneo yao ya ardhi kwa wastani wa sh 600,000 hadi sh milioni moja kwa wakala ambaye anadaiwa anataka kumuuzia maeneo hayo mwekezaji kutoka nchi za Uarabuni.


Kutokana na mwamko na uelewa mdogo wa wananchi, mawakala wamekuwa wakinufaika kwa kuuza viwanja hivyo kwa thamani kubwa ya kati ya sh milioni 150 hadi 200.


Hata hivyo, kuna wananchi wachache wamekuwa wakikataa kuuza maeneo yao na kutaka ardhi yao itumike kuwapatia hisa katika miradi inayotarajiwa kufunguliwa na wawekezaji hao.


Hali hiyo imejitokeza zaidi katika eneo lenye ukubwa wa hekta 30, ambalo awali SMZ ililiuza kwa Kampuni ya White Sand, lakini baadaye ikashindwa kuliendeleza na hivyo serikali kulichukua tena.


Kampuni hiyo inadaiwa ilishindwa kuliendeleza eneo hilo ambalo walikuwa wawekeze miradi ya kitalii, ikiwemo kufungua huduma za elimu pamoja na uwanja wa ndege.


Maeneo mengine yaliyokumbwa na migogoro ya ardhi na kuwagusa baadhi ya watu wazito ni Matemwe, Jambiani na Pwani Mchangani.


Mkurugenzi wa Mipango katika Kamisheni ya Utalii, Issa Mlingoti, naye alikiri kuwepo kwa matatizo katika sekta ya utalii yanayohusu migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wamiliki wa maeneo husika.


Alisema katika eneo la Matemwe, kumekuwa na mgogoro wa siku nyingi kati ya mwekezaji wa Hoteli ya Fairmont na wananchi, ambao wanataka wasiwekewe mipaka katika matumizi ya eneo hilo la hoteli katika shughuli zao za kijamii.


Mlingoti aliliambia gazeti hili kuwa, hali hiyo pia imejitokeza katika Hoteli ya Blue Bay na wanalazimika kuitisha vikao vya maelewano kati ya wananchi na wawekezaji ili kuondoa migigoro hiyo.


Maeneo mengine yaliyokumbwa na mgogoro wa ardhi ni mashamba ya Mziwanda yaliyoko Micheweni kisiwani Pemba ambako zaidi ya wakulima 50 wameathirika baada ya mashamba yao kuchukuliwa.


Mbali na eneo hilo, wananchi wa Mtangani, kisiwani Pemba nao wapo katika hali ya wasiwasi kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa kisiwa kimoja kiitwacho Kuji, kimepangwa kuchukuliwa kwa shughuli za uwekezaji, wakati ni shamba linalomilikiwa kihalali.


Wananchi hao wamesema wako tayari kuandamana iwapo shughuli za ujenzi zitaanza katika kisiwa hicho kwa vile kimekuwa tegemeo lao kubwa katika kujipatia riziki.


Aidha, familia moja ya eneo la Buyu, Wilaya ya Magharibi Unguja, pia imeingia katika mgogoro mkubwa na kigogo serikalini kwa madai kuwa amevamia eneo lao.


Uchunguzi zaidi unaonyesha kwamba, watu ambao walipaswa kusimamia sheria, badala yake wamekuwa sehemu ya wahusika wa migogoro hiyo na kuchangia matatizo mengi, ikiwemo uharibifu wa mazingira.


Hivi karibuni, Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid, alisema kwamba tayari ameteua timu ya wataalamu itakayopitia sera ya ardhi ili kuangalia mapungufu yaliyojitokeza na kufanya uchunguzi juu ya hali halisi ya matatizo ya ardhi nchini.


Mansour alisema kwamba Idara ya Ardhi imeteua kamati ndogo itakayofanya utafiti juu ya viwango vya kodi ya ardhi vinavyolipwa katika miradi ya uwekezaji.


Aidha, alisema kwamba serikali inaandaa mpango wa kuyahakiki upya maeneo ya ardhi yaliyotolewa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amani Karume kwa ajili ya shughuli za kilimo, ambapo hivi sasa wananchi wanayauza na kutumiwa kwa matumizi ambayo hayakukusudiwa.


Alisema kwamba katika kipindi cha 2006/07, miradi 16 imefutiwa mikataba ya ukodishwaji ardhi kutokana na wahusika kushindwa kuendeleza maeneo hayo.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents