Michezo

Arjen Robben atangaza kustaafu soka Uholanzi

Nahodha wa Uholanzi Arjen Robben ametanagza kwamba amestaafu soka ya kimataifa baada ya Uholanzi kushindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka ujao.

Robben alifunga mabao yote mawili katika ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Sweden, lakini mabao hayo hayakutosha kuwafikisha michuano ya kufuzu kwa muondoano.

Mshambuliaji huyo wa Bayern Munich alisema: “Haujakuwa uamuzi rahisi lakini sasa nina miaka 33 na nahitaji kuangazia zaidi klabu.”

Aliongeza, “Pia nahitaji kuonyesha makubwa zaidi katika vitu ambavyo naweza kuvifanya, na huu ndio wakati,”

Robben alichezea taifa lake mara ya kwanza Aprili 2003 na kwa jumla amewachezea mechi 96 na kufunga mabao 37.

Anashikilia nafasi ya nne kwenye ufungaji wa mabao timu ya taifa ya Uholanzi, nafasi anayoishikilia kwa pamoja na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Dennis Bergkamp.

Uholanzi walihitaji kushinda kwa mabao saba wazi dhidi ya Sweden ili kuwapita Sweden na kumaliza nafasi ya pili kundi lao.

Robben alikuwa kwenye kikosi kilichomaliza cha tatu Kombe la Dunia 2014 na kikosi kilichoshindwa fainali 2010 na Uhispania.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents