Askari kulipa nauli Dar, wanafunzi wapandishiwa nauli hadi Sh100

Dala dalaCHAMA cha Wamiliki wa Magari ya Abiria Mkoa wa Dar es Salaam (DARCOBOA), kimesema kinakamilisha taratibu za kuwatoza nauli askari wa majeshi yote nchini na kuongeza nauli ya wanafunzi kufikia Sh 100

Na Muhibu Said

CHAMA cha Wamiliki wa Magari ya Abiria Mkoa wa Dar es Salaam (DARCOBOA), kimesema kinakamilisha taratibu za kuwatoza nauli askari wa majeshi yote nchini na kuongeza nauli ya wanafunzi kufikia Sh 100 badala ya 50 wanayolipa hivi sasa.

Utaratibu wa askari kutolipa nauli kwenye daladala ambao haumo katika sheria wala katika maagizo ya wakuu wa majeshi, ulianzishwa miaka ya 1990 na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema.

Mwenyekiti wa DARCOBOA, Sabri Mabrouk, aliwaambia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa, wamefikia uamuzi huo kutokana na gharama za uendeshaji wa magari ya abiria kupanda maradufu.

“Hivi sasa makusanyo makubwa yanakwenda kwenye mafuta. Hivyo, askari watuonee huruma, waanze kujizoesha kulipa nauli. Wanafunzi nao wajitahidi kusoma shule zilizo jirani na wanakoishi, ndio ufumbuzi. Umefika umuhimu wa nauli kupanda. Sh 50 haina thamani miaka kumi iliyopita,” alisema Sabri na kusisitiza:

“Kulipa nauli kwa askari wa majeshi yote kunakuja, kwa sasa waanze kujizoesha.”

Kutokana na hali hiyo, alisema DARCOBOA imeiandikia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini nchini (SUMATRA) barua kuomba kukutana ili kujadili juu ya utekelezaji wa suala hilo mara moja.

Sabria alisema inashangaza kuona wanafunzi wanalipa nauli ya daladala, huku askari ambao wanafanya kazi na kulipwa mishahara wakiacha kulipa, lakini wanafanya hivyo kwenye mabasi yanayokwenda mikoani.

Hata hivyo, alisema ingawa sheria inataka wanafunzi walipe nusu ya nauli anayolipa mtu mzima, utafiti uliofanywa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) mwaka jana, umebaini kuwa wazazi na walezi wengi katika mikoa ya Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam, wako tayari kulipa nauli ya Sh 100.

Alisema wamelazimika kuwatoza askari na kuongeza nauli ya wanafunzi kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji wa magari kulikotokana na kushuka kwa thamani ya shilingi ambako, hali ambayo imesababisha uagizaji wa mafuta na vipuri vya gari kutoka nje ya nchi kuwa ghali zaidi.

Mwenyekiti, alisema bei ya mafuta aina ya dizeli, imepanda kutoka dola 60 (Sh 69,000) hadi kufikia dola 100 za Marekani (Sh 115,000) kwa pipa kwenye soko la dunia, mwaka huu.

Bei ya dizeli kwenye vituo vya Dar es Salaam, imepanda hadi kufikia Sh 1,755 kwa lita wiki iliyopita kutoka Sh 1,450 wiki za nyuma ambapo petroli imepanda hadi kufikia Sh 1,660 kutoka 1,500, wakati bei ya oil imepanda kutoka Sh 2,000 hadi 4,000 kwa lita na bei ya vilainishi na vipuri vya magari, imepanda zaidi.

Alisema bei ya tairi ya gari aina ya Toyota Hiace, imepanda kutoka Sh 25,000 hadi 70,000, huku bei ya kipuri hicho kwa gari aina ya Toyota DCM ikipanda kutoka Sh 55,000 hadi 110,000.

Sabri alisema la kusikitisha zaidi ni kuona bei ya Leseni ya Barabara kwa daladala imepanda kutoka Sh 20,000 hadi 330,000, wakati ya mabasi yanayokwenda mikoani imepanda kutoka Sh 20,000 hadi 175,000.

Aliwataka wamiliki wa daladala, kuwa na subira katika kipindi ambacho DARCOBOA inakamilisha taratibu za utekelezaji wa suala hilo.

Alisema bei ya mafuta aina ya dizeli, imepanda kutoka dola 60 (sawa na Sh69,000) hadi kufikia dola 100 (Sh 115,000) kwa pipa kwenye soko la dunia.

Mwenyekiti wa DARCOBOA Kanda ya Temeke, Mashaka Karume, aliwashauri wenye magari, yakiwamo ya serikali, Bunge na karandinga za polisi, kuwachukua wanafunzi ili kuwapunguzia adha ya usafiri.

Naye Katibu Mkuu wa DARCOBOA, Mujengi Jigwao, alisema anashangazwa na baadhi ya watu kwamba, gharama za makazi na bei ya vyakula zinapopanda, mambo huwa shwari, lakini nauli ya daladala inapopanda, hulalamika.

“Sisi si malaika, mahitaji yetu ni kama ya wengine,” alisema Jigwao.

Alishutumu tabia ya baadhi ya askari wa usalama wa barabarani ya kuwakamata wamiliki wa daladala kwa makosa yanayofanywa na madereva barabarani.

“Kitendo hicho hakina matokeo mema, kinaathiri abiria na wamiliki wa magari. Kinachotakiwa kila mtu abebe msalaba wake mwenyewe. Kwamba, makosa ya gari aadhibiwe mmiliki, lakini makosa ya utendaji, kama vile kukataa kuchukua wanafunzi, kuvuka taa nyekundu, kukata ruti, kutovaa sare, lugha chafu kwa abiria na uendeshaji mbaya, aadhibiwe dereva,” alisema Jigwao.

Akichangia hoja hiyo, Sabri alisema katika kikao kati yao na Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Waziri wa Mambo ya Ndani, kilichofanyika Mei 18, mwaka jana, waliikubaliana kwamba, makosa ya gari aadhibiwe mmiliki na makosa ya utendaji aadhibiwe dereva, kinyume na inavyofanywa hivi sasa.


 


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents