Atoa ushuhuda wa mauaji ya Rwanda

MSEMAJI wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Rwanda (ICTR), Roland Amoussouga jana aliwahuzunisha waandishi wa habari baada ya kuelezea alivyoshuhudia maiti za watu waliouawa nchini Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari

Na Mwandishi wa Habarii Leo 


 


MSEMAJI wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Rwanda (ICTR), Roland Amoussouga jana aliwahuzunisha waandishi wa habari baada ya kuelezea alivyoshuhudia maiti za watu waliouawa nchini Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994.

Amoussouga ambaye pia ni mshauri wa masuala ya sheria, alitoa ushuhuda huo wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, kuelezea maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji yaliyotokea Rwanda yaliyoanza Aprili 7 na yatahitimishwa kesho.

Msemaji huyo alipelekwa Rwanda na Umoja wa Mataifa akiwa na wenzake baada ya mauaji hayo ya watu zaidi ya 800,000 yaliyotokea kwa siku 100, ambako kazi yake ilikuwa kuhesabu maiti pamoja na kuchunguza mauaji yalivyotokea.

“Nilikuwa nikihesabu maiti na vichwa vya watu waliokufa, nilifanya kazi hiyo kwa takribani miaka miwili …kutokana na kuona hali hiyo ya watu walivyochinjwa niliacha kula nyama kwa miezi sita na kula mbogamboga tu…kuna siku niliangukia maiti na kuvunja mguu ambapo nililazimika kuvaa makubazi…,” alielezea.

Naye Balozi wa Rwanda nchini, Zeno Mutimura amesema mauaji ya kimbari yaliyotokece: a nchini kwake yalisababishwa na uongozi mbaya wa viongozi waliopita wa nchi hiyo na kuongeza; “Mfano Rais Juvenal Habyarimana aliwahi kuulizwa anavyojisikia juu ya wakimbizi milioni 2.1 waliotawanyika katika nchi jirani kwa miaka 20, alijibu kuwa ‘waambie wakae huko huko, nchi hii ni ndogo kuweza kuwachukua’.

Wakati huohuo, ubalozi huo wa Rwanda kwa kushirikiana na ofisi za Umoja wa Mataifa nchini umeandaa mjadala wa wazi utakaofanyika kesho Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM). Rais wa Chama cha Haki za Binadamu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bakari George alisema siku hiyo kutakuwa na mijadala mbalimbali itakayotolewa na watu mbalimbali akiwamo Mkurugenzi wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku na Profesa Mweisiga Baregu.


 


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents