Azikwa juu ya kaburi lingine mkono nje

Mwili wa mtu asiyefahamika umezikwa juu ya kaburi la mtoto wa Mchungaji huku mkono wake mmoja ukiwa umebaki nje, tukio hilo la aina yake limevuta hisia za wakazi wa kitongoji cha Mbalizi nje kidogo ya jiji la Mbeya.

Mwili wa mtu asiyefahamika umezikwa juu ya kaburi la mtoto wa Mchungaji huku mkono wake mmoja ukiwa umebaki nje, tukio hilo la aina yake limevuta hisia za wakazi wa kitongoji cha Mbalizi nje kidogo ya jiji la Mbeya.

Kaburi hilo ambalo awali lilizikwa mwili wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Oliver Adam (30) ambaye ni mtoto wa Mchungaji wa Kanisa la Kibaptisti aliyefariki dunia Juni 8 mwaka huu, lilikutwa likiwa limefukiwa mtu mwingine ambaye hakufahamika mara moja.

Mwili wa mtu huyo juzi ulikutwa ukiwa umekatwa mikono yote miwili na vidole viwili huku mkono mmoja ukionekana nje ya kaburi hilo. Akizungumzia kadhia hiyo mbele ya waandishi wa habari nyumbani kwake jana, baba wa marehemu Oliver Mchungaji Adamu Mwanyika (55) alisema alifuatwa na Bw.

Andulile Mwalyondo, ili kujua kama aliwahi kutembelea eneo alilozikwa mwanawe hivi karibuni. Alisema Bw. Mwalyondo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo, alimtaka waongozane hadi makaburini, ili ashuhudie kilichopo juu ya kaburi la mwanawe Juni 18 mwaka huu.

Mchungaji Mwanyika alisema walipofika eneo la makaburini alikuta umati wa watu umefurika kuzunguka kaburi hilo ambapo aliuona mkono ukiwa umechomoza nje ya kaburi la mwanawe.

Alisema hali hiyo ilileta tafrani kutokana na kuwapo hisia za ushirikina ambapo alichukuliwa hadi kituo kidogo cha Polisi Mbalizi kwa mahojiano zaidi.

Alifafanua kuwa alipofika kituoni alithibitisha kuwa lile lilikuwa ni kaburi la mwanawe na kwamba alikuwa hana uhakika kama mkono uliokuwa ukichungulia juu ya kaburi ulikuwa ni wa marehemu mwanawe.

Mchungaji Mwanyika alidai kuwa ilitolewa amri ya kulifukua kaburi hilo baada ya mawasiliano na Mganga Mkuu wa Mkoa na Hakimu Mkazi wa Wilaya.

Alisema katika maswali aliyoulizwa ni pamoja na kujua urefu wa kaburi ambalo lilikuwa futi saba na namna ambavyo marehemu alizikwa, ambapo aliwaeleza kuwa alizikwa ndani ya sanduku la mbao kwa ibada iliyoongozwa na Mchungaji Admini Mbembela wa Kanisa la Moravian Usharika wa Yeriko.

Alisema amri ya kufukua kaburi hilo, ilitolewa na saa 12 jioni kaburi lilifukuliwa na kukutwa mwili wa mwanaume asiyefahamika.

Aidha, alisema wakati wa ufukuaji wa kaburi ukiendelea pembeni mwake kulionekana miburuzo ya matairi ya toroli ambayo yaliashiria kutumika kuubeba mwili wa marehemu huyo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Emmanuel Kabwogi, alisema hajaletewa taarifa hizo na kuahidi kuwa atazitoa kwa waandishi mara baada ya kupata vielelezo vya kutosha.

 

 

 

 

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents