Habari

Balaa kubwa Anglikana

KATIKA hatua inayoonyesha kukua kwa mgogoro ndani ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma, waumini wa kanisa hilo wanaompinga askofu wao wamelisambaratisha kanisa lao.

na Mwandishi Wetu, Ruvuma


KATIKA hatua inayoonyesha kukua kwa mgogoro ndani ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma, waumini wa kanisa hilo wanaompinga askofu wao wamelisambaratisha kanisa lao.


Kanisa hilo ambalo liko Mtaa wa Chiulu, Mbamba Bay, limesambaratishwa vibaya sehemu yake ya madhabahu pamoja na kuondelewa kwa vifaa muhimu vinavyotumiwa na Askofu Dk. Maternus Kapinga, wakati wa kuendesha ibada.


Watu walioshuhudia tukio hilo ambalo si la kawaida katika historia ya kanisa hilo, walieleza kuwa waumini wenye hasira walivamia kanisa hilo na kuvunjavunja madhabahu, kisha wakaondoa kiti cha askofu wao, ambacho hukitumia kuketi wakati akiendesha ibada.


Mashuhuda hao walieleza kuwa mbali na kiti hicho cha askofu, pia waumini hao waliondoa mavazi rasmi yanayotumiwa na mapadri, mashemasi na walimu wa dini wakati wakiendesha ibada.


Kwa mujibu wa habari hizo, hatua hiyo inalenga kumzuia Askofu Dk. Kapinga kutoa sakramenti ya Kipaimara kwa watoto na waumini wa kanisa hilo wanaoishi katika mtaa huo.


Katibu wa sinodi ya dayosisi hiyo, James Lombola, alilieleza gazeti hili hatua hiyo ya waumini ni ishara kwamba wamechoshwa na ukimya wa muda mrefu kutoka mamlaka ya juu ya kanisa hilo.


“Hii ni ishara ya kuzuia huduma za aina yoyote za kiroho zilizotakiwa kutolewa na Askofu Dk. Kapinga, na kwa hali hiyo wamemkataa asiendelee na kazi ya uaskofu wa kanisa letu,” alisema Lombola.


Alisema waumini hao waliwasilisha malalamiko ya kumkataa Askofu Dk. Kapinga kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Donald Mtetemela, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa kurejesha amani.


“Nimepata taarifa za kuaminika kuwa waumini wa Kanisa la Chiulu wamechukua uamuzi wa kuvunja ‘vestori’ na kuondoa vitu muhimu, ikiwa ni pamoja na kiti cha askofu, mavazi yake na vifaa vya misa takatifu,” alisema Lombola.


Aliongeza kwamba baada ya waumini kuchukua hatua hiyo, sasa Askofu Dk. Kapinga, hataweza tena kutoa huduma hiyo katika Kanisa la Chiulu, badala yake habari zimesema anataka kuhamishia huduma hiyo katika kanisa jingine lililopo katika Kijiji cha Kwambe, umbali wa km 20 kutoka Chiulu.


Habari zaidi zimesema kwamba, askofu Dk. Kapinga alifika katika Kijiji cha Chiulu akiwa na askari polisi wenye silaha, ikiwa ni jitihada zake za kujaribu kushinikiza kuendesha ibada kwa nguvu.


Kwamba, msafara wa askofu huyo, uliwasili katika kijiji hicho ukiwa na magari ya askari polisi wenye silaha waliokuwa wakimlinda lakini alishindwa kuendelea na ibada baada ya kukuta madhabahu yamevunjwa, kiti na mavazi yake vikiwa vimeondolewa.


Askofu Kapinga mwenyewe hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia suala hili, kama ilivyo kwa Dk. Mtetemela, ambaye kanisa lake ‘linaloandamwa’ na kashfa ya ushoga duniani, pia liko katika fukuto mkoani Dodoma.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents