Barabara Arusha kukwaza Mkutano wa Sullivan

Barabara za ArushaWAKATI Tanzania inatarajia kupokea idadi kubwa ya wageni kutoka Marekani wakati wa Mkutano wa Leon Sullivan, utakaofanyika mjini hapa mwezi ujao, hali ya barabara bado ni tatizo kubwa


 



Barabara za Arusha

 

na Richard Mwangulube, MAELEZO, Arusha




WAKATI Tanzania inatarajia kupokea idadi kubwa ya wageni kutoka Marekani wakati wa Mkutano wa Leon Sullivan, utakaofanyika mjini hapa mwezi ujao, hali ya barabara bado ni tatizo kubwa.

Ufinyu wa barabara na kutofunguliwa kwa barabara mpya ili kukabili ongezeko la magari, kumeendelea kusababisha msongamano wa magari katika barabara chache mjini hapa.

Hali hiyo pia imezidi kuwa mbaya baada ya kuvunjika kwa madaraja makubwa matatu muhimu katika kusaidia kupunguza msongamano wa magari katika jiji hili.

Madaraja hayo hayajatengemaa licha ya juhudi za serikali kuipatia Manispaa ya Arusha fedha za kuhakikisha madaraja yote matatu muhimu yaliyobomolewa na mvua zinazoendelea, yanatengenezwa kwa haraka kabla ya mkutano huo unaolenga kusaidia kukuza sekta ya utalii na biashara.

Mkutano wa Sullivan unatarajia kuwaleta watu zaidi 3,500 wenye asili ya Marekani.

Kutokamilika kwa madaraja hayo, hasa lile la Mto Naura, linalounganisha ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na makao makuu ya polisi mkoani hapa, kunakwamisha usafiri na usafirishaji katika Manispaa ya Arusha na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.

Baadhi ya watu waliohojiwa jana wakati ujenzi wa daraja la Mto Naura unaendelea, walisema hakukuwa na sababu kwa mkandarasi aliyepewa kazi hiyo kulivunja kabisa daraja hilo na badala yake angeweza kuliimarisha zaidi.

Akizungumzia hali hiyo, mwananchi mmoja mhandisi mstaafu anayeishi hapa, John Mollel, aliishauri serikali kuongeza nguvu zaidi kwa kuleta Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kumalizia ujenzi wa daraja hilo, ili kunusuru hali hiyo inayoweza kulisababishia taifa aibu.

“Iwapo mkandarasi huyo ataachiwa kazi hiyo huenda asiimalize kabisa kazi ya kujenga daraja hilo muhimu kabla ya kuanza kwa mkutano huo,” alifafanua.

Naye Veronica Elias, mkazi wa Sanawari, hapa, alishauri Wakala wa Barabara kuingilia kati ujenzi wa daraja hilo kutokana na Manispa ya Arusha kutokuwa na uwezo pamoja na mkandarasi aliyepewea kazi kufanya kazi yake kwa kusuasua.

Wajumbe wa mkutano wa Sullivan wanatarajia kuanza kuwasili mkoani Arusha mwishoni mwa mwezi huu wakati mkutano mwingine wa dunia wa utalii unatarajia kufanyika kabla ya mkutano wa Sullivan utakaowajumuisha watu zaidi ya 4,000.


 


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents