Habari

Barabara njia tatu Dar mvurugano

MAJARIBIO ya agizo la Waziri Mkuu, Edward Lowassa la baadhi ya barabara kupitisha mistari mitatu ya magari badala ya mawili, yamezua kizaazaa barabarani.

Halima Mlacha


MAJARIBIO ya agizo la Waziri Mkuu, Edward Lowassa la baadhi ya barabara kupitisha mistari mitatu ya magari badala ya mawili, yamezua kizaazaa barabarani. Kizaazaa cha majaribio hayo yaliyoanza jana, kilitokana na watumiaji wengi wa barabara hizo kutokuwa na taarifa kamili za majaribio hayo hivyo kujikuta wakikutana uso kwa uso na magari ya mwelekeo mwingine.


HabariLeo jana asubuhi lilishuhudia msongamano wa magari katika barabara mbili za Ali Hassan Mwinyi na Morogoro, ambazo utaratibu huo ulianza rasmi kwa majaribio. Baadhi ya madereva walionyesha kutokuwa na taarifa za kuwapo kwa matumizi ya njia tatu, kwani walikuwa wakibisha na kuendelea kuendesha katika njia wasiyotakiwa, hali iliyoleta hatari ya kutokea ajali.


Katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi gazeti hili lilishuhudia ajali zaidi ya mbili za magari kukwaruzana na magari mengine kunusurika kugongana uso kwa uso baada ya askari kuyaelekeza magari yanayoenda mjini kutumia njia tatu. Katika barabara ya Morogoro baadhi ya madereva walifikia kutukanana wakifikiri kuwa wenzao walikuwa wanafanya fujo na kuvunja sheria, hali iliyosababisha ubishi na msongamano mkubwa wa magari.


Pamoja na hayo, gazeti hili lilishuhudia wingi wa askari wa Usalama wa Barabarani katika barabara hizo wakijitahidi kuongoza magari, hali ambayo kwa kiwango fulani ilisaidia kuleta uelewa kwa baadhi ya madereva juu ya majaribio hayo. Katika barabara ya Morogoro, mmoja wa abiria, Kanaeli Kaale alisema alishuhudia mkanganyiko uliokuwapo kati ya madereva wenyewe na watembea kwa miguu, kwani wengi wao walionekana kuushangaa utaratibu huo mpya.


“Ni wazi kuwa watu hawana taarifa ya kuanza kwa matumizi ya njia tatu, kwani watembea kwa miguu wengi wamenusurika kugongwa na magari yenyewe yamenusurika kugongana,” alisema Kaanaeli.


Alisema mkanganyiko ulionekana kuongezeka zaidi kwa daladala ambazo zilikuwa zikitumia njia ya akiba ya upande mwingine wa barabara, kutokana na kutokuwa na vituo vya kushushia abiria, hali iliyosababisha daladala kusimama na kushusha abiria katikati ya barabara na hivyo kuongeza msongamano wa magari. Naye mmoja wa trafiki katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, alisema utaratibu huo umeleta kizaazaa kutokana na ukweli kuwa madereva wengi na watembea kwa miguu hawakuwa na taarifa ya kuanza kwake.


Alisema hali ilizidi kuwa mbaya saa 2:00 asubuhi, kwani mkanganyiko huo ulisababisha foleni ndefu kwenye barabara ya magari yanayotoka mjini ambayo yalitakiwa kutumia njia moja.


Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani Taifa, James Kombe, alisema kwa sasa ni mapema mno kuuzungumzia utaratibu huo kwani ndiyo kwanza unaanza kutekelezwa. “Ni mapema mno kusema chochote leo (jana) kwani majaribio ya agizo la Waziri Mkuu yameanza katika barabara mbili tu za Ali Hassan Mwinyi na Morogoro,” alisema Kombe.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents