Habari

Bila tume huru wapinzani wasahau kuingia Ikulu – Kingunge

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amesema bila ya kuwa na tume huru ya uchaguzi na katiba mpya, vyama vya upinzani visahau kushinda urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Kauli ya mwanasiasa huyo mkongwe imekuja siku moja baada Rais John Magufuli kumteua Jaji Themistocles Kaijage kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya Jaji Damian Lubuva kufikia muda wake wa kustaafu.

Kwa muda mrefu, NEC imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kwa kutokuwa huru kwa sababu ya uongozi wake wote huteuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, huku sheria zikikataza matokeo ya nafasi ya urais kupingwa mahakamani.

Akizungumza katika mkutano wa kuwafariji vijana waliokamatwa na Jeshi la Polisi na kushtakiwa kwa makosa yaliyohusu Uchaguzi Mkuu uliopita, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Kingunge aliwatia moyo vijana hao, akisema hakuna ushindi unaopatikana bila kupambana.

“Yako mambo ambayo itabidi tujitahidi yaamuliwe sasa kabla ya 2020. Mambo hayo makubwa kwanza ni tume huru (ya uchaguzi). Suala hilo lazima lizungumzwe sasa, hatuwezi kwenda 2020 na tume ya sasa na Katiba ya mwaka 1977, tukienda hivyo sahau habari ya upinzani kushinda uchaguzi,” alisema Kingunge.

“Sheria inayohusu matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa. Hivi sasa sheria inasema matokeo ya uchaguzi wa Rais hayahojiwi mahakamani. Lazima hilo suala lipate jibu sasa. Kwa hiyo Katiba na sheria iseme, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kuhojiwa mahakamani. Tusipokuwa na hilo, tutakuwa na matatizo makubwa sana”.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents