Habari

Binti ahama kwao kukwepa kuozwa

Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Ilkerin, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, amelazimika kutoroka nyumbani kwa wazazi wake kukwepa kuozwa kwa nguvu.

Na Novatus Makunga, PST Arusha

 
Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Ilkerin, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, amelazimika kutoroka nyumbani kwa wazazi wake kukwepa kuozwa kwa nguvu.

 

Mwanafunzi huyo, Sindani Logelleki (13), alidai kuwa, hiyo ilikuwa ni mara ya pili kukimbia na kwenda kujihifadhi kwa msamaria mmoja akikwepa kuozwa kwa nguvu.

 

Alisema mara ya kwanza ilikuwa wakati wa Sikukuu ya Krismasi, mwaka jana.

 

Mwanafunzi huyo ambaye ana maendeleo mazuri darasani, alisema wakati wa Krismasi, alikimbilia ofisi ya kijiji cha Ngurboko na alihifadhiwa nyumbani kwa ofisa Mtendaji wa kijiji hicho kwa siku tatu.

 

“Nililala nyumbani kwa mtendaji wa kijiji kwa siku tatu mpaka viongozi wa kijiji walivyomwita baba na kumlazimisha kurudisha bangiri na vitu vingine alivyochukua kama mahari kwa lengo la kunioza,“ alieleza mwanafunzi.

 

Sindani alisema tukio la pili lilitokea katikati ya mwezi uliopita ambapo kijana aliyetaka kumuoa alikwenda nyumbani kwao.

 

Hata hivyo, alisema alifanikiwa kukimbilia katika viwanja ambavyo madhehebu ya moja ya dini huendesha mahubiri kila Jumapili, eneo la jirani la Kisongo.

 

Alisema pamoja na kukimbia, baba yake aliwapa baiskeli vijana wawili wamfuatilie na kumkamata lakini walishindwa kutokana na msaada alioupata wa waumini ambao walimuomba mwanamke mmoja ambaye pia Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kisongo, Bi. Cobnita Naivasha, kumpa hifadhi.

 

Alidai kuwa, alishindwa kupata msaada mkubwa kutoka kwa uongozi wa kijiji ambao alidai upo karibu mno na baba yake na ndiyo maana hakurudi tena ofisi ya kijiji na badala yake aliamua kikimbilia kanisani.

 

Kwa upande wake, Bi. Naivasha alieleza kuwa, baada ya kuelezwa mkasa huo, alimuonea huruma binti huyo na kuamua kumpa hifadhi wakati suluhisho la tatizo hilo likitafutwa baina ya serikali ya kijiji, shule, mtoto mwenyewe na mzazi.

 

“Niliombwa na binti mmoja ambaye ni muumini wa madhehebu hayo, Bi. Matilda Kilenga baada ya kuona mtoto yule akifukuzwa na watu wawili waliokuwa na baiskeli,“ alifafanua.

 

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Bernard Mchallah, alisema taarifa za kukimbia kwa mtoto huyo nyumbani kwa wazazi wake, alipewa na uongozi wa kijiji hicho.

 

“Ni kweli nimepewa taarifa na uongozi wa kijiji na nilipoenda kuangalia rejesta ya mahudhurio darasani nikagundua kuwa Sindani hakuja kwa siku mbili darasani wakati mahudhurio yake siku zote ni mazuri,“ alifafanua.

 

Hata hivyo, baba mzazi wa mtoto huyo, Bw. Logelleki Shivava Lemunge, alikataa madai ya kutaka kumuoza binti yake na kwamba hakuchukua mahari kutoka kwa mwanaume yeyote.

 

“Huyo mtoto amekimbia nyumbani kwa kuwa namzuia kwenda kusali katika Kanisa la Upako kwani akienda huko, hukosa kwenda shule na mara nyingine hulala huko huko kwa muda wa siku tatu,“ alidai Bw. Lemunge.

 

Hata hivyo, alishindwa kutoa ufafanuzi wa jinsi gani mtoto ambaye anakwepa shule kwa kwenda katika mahubiri yanayoendeshwa kila Jumapili huku akiwa na mahudhurio mazuri darasani na kufanya vizuri kwa kushika nafasi ya sita kimasomo.

 

Na hata alivyobanwa zaidi kwa upande wa posa iliyodaiwa kupokelewa mwishoni mwa mwaka jana, alidai kuwa yeye hakuwepo nyumbani bali alikwenda wilayani Kiteto na kudai labda aliyefanya hivyo ni mdogo wake ambaye alikataa kumtaja jina.

 

Mwenyekiti wa kijiji ambacho shule hiyo ipo cha Ngurboko, Bw. Saivoyi Naigisa alithibitisha hatua ya baba wa mtoto huyo kupokea bangiri na vitu vingine kama posa mwishoni mwa mwaka jana, lakini alisema uongozi wa kijiji ulimwamuru kurudisha mara moja ili mtoto aweze kumaliza shule.

 

“Tulimwita baada ya binti kukimbilia ofisi ya kijiji na huyo mzee alituahidi kwamba atarudisha kila kitu alichochukuwa na kwamba hatamuoza tena binti yake.

 

Mbali ya binti huyo, tayari kuna madai kuwa, katika darasa la saba la shule hiyo lenye jumla ya wanafunzi 42 ni watoto sita tu wa kike ambao hawajatafutiwa wachumba.

 

Hata hivyo, si viongozi wa kijiji hicho wala wa shule waliokuwa tayari kuliweka bayana suala hilo ingawa wanafunzi wenyewe walisema.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents