Habari

Bucha zafungwa, kuku wapaa

BAADHI ya bucha zinazouza nyama ya ng’ombe katika Jiji la Dar es Salaam, zimefungwa kutokana na kukosa wateja katika kipindi cha Sikukuu ya Pasaka.

na Edmund Mihale


BAADHI ya bucha zinazouza nyama ya ng’ombe katika Jiji la Dar es Salaam, zimefungwa kutokana na kukosa wateja katika kipindi cha Sikukuu ya Pasaka.



Hatua hiyo imekuja baada ya wateja wengi watumiao kitoweo hicho kuhofia kupata maambukizi ya ugonjwa wa homa ya bonde la ufa (RVF).



Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima jana, umebaini kuwa pamoja na kupendwa kwa kitoweo hicho kutumiwa katika sikukuu mbalimbali, hali imekuwa ngumu kibiashara katika kipindi hiki cha Pasaka kinyume cha miaka mingine.



Uchunguzi huo umebaini kufungwa kwa baadhi ya bucha katika maeneo ya Ubungo Kibangu, Ubungo Kisiwani, Ubungo Maji, Kinondoni, Kariakoo, Tabata na Temeke.



Wakizungumza na Tanzania Daima, baadhi ya wamiliki wa bucha hizo, wamesema hawako tayari kuendelea kufanya biashara hiyo hadi ugonjwa huu utakapopatiwa ufumbuzi.



“Nimekuwa nikipata hasara kila siku kutokana na kulaza kiasi kikubwa cha nyama tangu ugonjwa huu uripotiwe, hivyo siwezi kuendelea kuleta nyama, ni bora niangalie biashara nyingine hadi hapo ufumbuzi wa ugonjwa utakapopatikana,” alisema mmiliki wa bucha eneo la Kinondoni, aliyejitambulisha kwa jina moja la Hussein.



Naye mmiliki mwengine aliyejulikana kwa jina moja la Msafwa katika eneo la Ubungo Kibangu, alisema biashara hiyo imekuwa ngumu hali inayompa wakati mgumu wa kushindwa hata kuwalipa wafanyakazi wake.



Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa akina mama waliokutwa na Tanzania Daima katika maeneo ya Soko la Kariakoo ambako walionekana kutafuta kitoweo hicho huku na kule bila ya mafanikio.



“Mimi nimetoka maeneo ya Ubungo nikitarajia kupata mahitaji yangu yote ya Pasaka huku Kariakoo, lakini nimekwama kupata nyama na sasa naambiwa labda nijaribu maeneo ya Tabata,” alisema mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Tausi, mkazi wa Ubungo.



Mpaka sasa ugonjwa huu umeripotiwa kuua watu zaidi ya 40 nchini.



Wakati huohuo, Ratifa Baranyikwa, anaripoti kuwa, bei ya kuku imepanda maradufu jijini Dar es Salaam kutokana na kuongezeka kwa mahitaji baada ya watu kuacha kula nyama ya ng’ombe wakihofia ugonjwa wa RVF.



Utafiti uliofanywa na Tanzania Daima katika sehemu tofauti jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa kuku mmoja wa kisasa huuzwa kati ya sh 7,000 hadi sh 9,000 badala ya bei ya awali ya sh 2,500 hadi sh 3,000.



Hata hivyo, kuku hao wanauzwa wakiwa wadogo, hivyo kuhatarisha afya za walaji kwa kuwa wanakuzwa kwa dawa.



Aidha, kuku wa kienyeji nao wamepanda kwa asilimia 70 na hivi sasa kuku mmoja huuzwa kati ya sh 10,000 hadi 15,000.



Hata hivyo, wakazi wengi wa jijini Dar es Salaam waliozungumza na Tanzania Daima, walisema kuwa ipo haja Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, iwabane wale wote wanaosambaza kuku hao wakiwa wadogo.



Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents