Bunge la Lebanon leo limeidhinisha hali ya dharura katika mji mkuu Beirut katika kikao chake cha kwanza tangu mlipuko uliosababisha vifo na hasara kubwa wiki iliyopita.
Idhinisho hilo linalipa jeshi la nchi hiyo nguvu kubwa wakati ambapo ghadhabu miongoni mwa wananchi zinazidi na mustakabali wa kisiasa nchini humo ukiwa haubainiki.
Kabla kujiuzulu serikali ya Lebanon ilikuwa imetangaza hali hiyo ya dharura ingawa ilikuwa inahitaji kuidhinishwa na bunge.
Hatua hiyo imekosolewa na makundi ya kutetea haki za binadamu na wakosoaji wengine wanaosema serikali ya kiraia tayari ilikuwa inatumia nguvu dhidi ya waandamanaji kwa sababu ya janga la virusi vya corona.
Bunge la Lebanon linafanya vikao vyake katika eneo lengine mbali na bunge kwa ajili ya kuweka umbali wa mtu hadi mtu kutokana na virusi vya corona na pia raia wa nchi hiyo wamekusanyika nje ya bunge wakiandamana na kutaka wanasiasa wote waachie ngazi.