Choki: Hatuna uhasama na Chipolopolo

Ali Choki amesema Twanga Pepeta haina uhasama na Twanga Chipolopolo kama ambavyo imekuwa ikidhaniwa.


2006-03-19 08:59:10
By George John

Ali Choki amesema Twanga Pepeta haina uhasama na Twanga Chipolopolo kama ambavyo imekuwa ikidhaniwa.

”Ni mawazo ya watu tu kwamba tuna uhasama… Chipolopolo ni wenzetu kwa kuwa ni watoto wa mama mmoja na ndio maana tunafanya kazi pamoja,”alisema akizungumzia matukio kadhaa ya rapa wa Chipolopolo Msafiri Diouf kupanda katika jukwaa lao la Twanga Pepeta.

Choki amesema hisia kwamba bendi hizo zina uhasama licha ya kumilikiwa na kampuni moja ya ASET zinatoka kwa wasioitakia mema African Stars Entertainment.

”Wanapoona kuwa bendi zimeamua kufanya kazi kiushindani wanaamua kusema kuwa kuna uhasama… wanashindwa kutofautisha ushindani na uhasama,” alisema muimbaji huyo nyota aliyerejea Twanga Pepeta akitokea Mchinga Generation G8.

Aidha, Choki amesema anafurahia kuibuka upya kwa bendi hiyo ambayo ilianguka tangu alipoondoka Mwinjuma Muumin wakati alipotamba na kibao cha ‘Tunda’.

”Inafurahisha kuona African Revolution (Chipolopolo) sasa inafanya kazi tena kiushindani kama zamani kwasababu wengi waliitabiria kifo,” alisema Choki kuizungumzia bendi hiyo iliyopata nguvu mpya baada ya kujiunga kwa wanamuziki nyota waliotokea Twanga Pepeta wakiongozwa na Banzastone na Diouf.

Tangu kuibuka kwa Chipolopolo kumekuwepo na madai kwamba bendi hizo zina uhasama, jambo ambalo Choki anasema halina ukweli.

”Kama watoto wa familia moja mnagombana ndani ya nyumba… tabia hiyo utaiitaje?” alisema Choki ambaye tangu ajiunge kundini African Stars ameshaibuka na tungo mbili za ‘Password ya Maisha’ na ‘Maisha ya Ndoa’.

  • SOURCE: Lete Raha

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW