Habari

Elimu sekondari iwe bure – Bwana Mapesa

Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), Bw. John Cheyo, maarufu pia kama Bwana Mapesa, ameishauri serikali itoe elimu ya sekondari bure ili kila Mtanzania afike kidato cha nne.

Na Joseph Mwendapole

 
Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), Bw. John Cheyo, maarufu pia kama Bwana Mapesa, ameishauri serikali itoe elimu ya sekondari bure ili kila Mtanzania afike kidato cha nne.

 

Alitoa ushauri huo jana Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujenzi wa shule za sekondari katika jimbo lake.

 

Alisema serikali inaweza kutekeleza ushauri huo endapo itaweka mipango mizuri ya muda mrefu.

 

Bw. Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha UDP Taifa, alisema bila kufanya hivyo, Watanzania watashindwa kukabiliana na ushindani mkubwa uliopo katika dunia ya sasa ya utandawazi.

 

`Kwa dunia ilivyo sasa elimu ya msingi haitoshi kabisa. Tuweke msisitizo katika kusomesha watu wetu ili waweze kuhimili ushindani katika karne hii ya sayansi na teknolojia,` alisema Bw. Cheyo.

 

Aidha, Bw. Cheyo aliitaka serikali kuacha kufanya mambo yake kwa mtindo wa kushtukiza kama ambavyo inafanyika hivi sasa katika ujenzi wa shule za sekondari.

 

Alisema badala yake, inapaswa kuwa na takwimu za wanafunzi wanaotarajiwa kumaliza shule za msingi kila mwaka na kutenga fungu la kuongeza shule na idadi ya vyumba vya madarasa.

 

Alisema kwa kufanya mambo kwa kushtukiza, uko uwezekano wa kujenga majengo yasiyo na ubora unaotakiwa hivyo kuhatarisha maisha ya wanafunzi watakaotumia vyumba hivyo.

 

`Wanatakiwa kujua mwakani wanafunzi kadhaa wanamaliza na watahitaji shilingi ngapi, madarasa mangapi kisha kutenga bajeti, sasa tutaendelea na mtindo wa zimamoto mpaka lini,` alihoji Bw. Cheyo maarufu kama `Bwana Mapesa`.

 

Alisema katika jimbo lake la Bariadi Mashariki, wananchi wamehamasika na wamejenga kwa nguvu zao shule mpya 43 za sekondari, zenye thamani ya Sh. bilioni nne.

 

Alisema shule hizo zitafunguliwa mwezi Machi mwaka huu na wanafunzi waliofaulu na kukosa nafasi za kuingia kidato cha kwanza watapata nafasi.

 

`Kwa kweli nawapongeza wananchi wa Bariadi kwa kuona kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha na kuamua kujenga shule nzuri na imara,` alisema Bw. Cheyo.

 

Hata hivyo, Bw. Cheyo alisema anakerwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali wanaowanyanyasa wananchi kwa kuwalazimisha kutoa michango ya elimu, ili hali wameshaonyesha moyo wa kujitolea.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents