Habari

Familia ya Nyerere yaigomea serikali

SAKATA la kubomoa nyumba ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, eneo la Magomeni maduka sita, Dar es Salaam, limeingia katika sura mpya baada ya familia yake kuitaka serikali kusitisha azima hiyo na badala yake iwe chini ya Makumbusho ya Taifa.

na Irene Mark


SAKATA la kubomoa nyumba ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, eneo la Magomeni maduka sita, Dar es Salaam, limeingia katika sura mpya baada ya familia yake kuitaka serikali kusitisha azima hiyo na badala yake iwe chini ya Makumbusho ya Taifa.


Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Madaraka Nyerere, ambaye ni mtoto na msemaji wa familia ya Mwalimu, alihoji sababu za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kutaka kubomoa nyumba hiyo aliyowahi kuishi Baba wa Taifa wakati wa harakati za kutafuta uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, miaka ya 1957 akiwa Rais wa TANU.


Mwalimu Nyerere, aliishi kwenye nyumba namba nne iliyopo kwenye mstari mmoja unaounganisha nyumba sita na aliishi humo kwa miaka minne kabla ya kumwachia mama yake mzazi.


Madaraka, alisema haoni sababu ya NHC kuchukua uamuzi huo alioutafsiri kama uharibifu na upotevu wa kumbukumbu muhimu za taifa.


Uamuzi wa kubomoa nyumba hizo utaanza Julai mosi mwaka huu, baada ya kumalizika kwa muda wa miezi sita waliopewa wapangaji wa nyumba hizo na kupisha ujenzi wa ghorofa la kisasa.


“Kwa niaba ya familia ya Mwalimu…naiomba serikali isitishe uamuzi huo, tumesikia kuwa nyumba ile inataka kubomelewa, sisi hatutaki. Tunataka iachwe kama ilivyo kwa nia ya kuihifadhi.


“Hakuna sababu ya kubomoa, swali jingine la kujiuliza, kama wanataka kujenga, nchi hii ina kilometa za mraba zaidi ya 900,000, hivi wamekosa kweli sehemu ya kujenga ila kubomoa nyumba ya kumbukumbu?” alihoji Madaraka.


“Ukweli sisi wana familia hatutaki kabisa kunanihii…hiyo nyumba ibaki kama kumbukumbu ya Mwalimu kwa ajili ya vizazi vijavyo,” alisema.


Aidha, msemaji huyo aliwataka viongozi wa juu serikalini kuliangalia upya suala hilo kwa kuwataka wahusika wa mpango wa kubomoa nyumba hiyo wasitishe haraka uamuzi wao.


Hata hivyo, NHC ilitoa taarifa ya miezi sita ya kutaka familia sita zinazoishi kwenye nyumba hiyo kuhama ifikapo Juni 30 mwaka huu kwa maelezo kuwa panatakiwa kujengwa ghorofa.


“Tumepewa notisi ya miezi sita kuanzia Januari mosi hadi mwisho wa mwezi huu…katika notisi hiyo tumeelezwa kuwa ikifika Julai mosi panawekwa uzio tayari kwa kubomolewa,” alisema mmoja wa wapangaji.


Kwa mujibu wa sheria ya Jamhuri namba 10 ya mwaka 1964 na marekebisho yake namba 22 ya mwaka 1979, maeneo ya kumbukumbu hukabidhiwa Idara ya Mambo ya Kale chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.


Dhumuni la sheria hiyo ni kuhifadhi, kuenzi na kutunza maeneo na vitu muhimu vya wanasiasa, viongozi maarufu wenye mchango katika ustawi na maendeleo ya taifa.


Septemba 22 mwaka jana, Serikali ilitoa tangazo namba 135 likionyesha kuwa majengo na maeneo 193 ya kumbukumbu nchi nzima yatahifadhiwa na kulindwa kwa mujibu wa sheria.


Ndani ya kipindi cha miezi sita baada ya tangazo la serikali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Jumanne Maghembe, alitoa tangazo jingine namba 51 la Machi 2 mwaka huu linaloonyesha kufutwa kwa tangazo la awali.


Hivyo basi, tangazo lililotolewa na Waziri Maghembe liliidhinisha kubomolewa kwa majengo ya kale yenye kumbukumbu muhimu, hali inayopingwa na wahifadhi wa mambo ya kale kwa kile wanachodai kuwa ni kupoteza historia ya nchi kwa vizazi vijavyo.


Souce: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents