Habari

Gari Dar lavaa kituo cha polisi

Gari moja Jijini limekifumua kituo kidogo cha Polisi na kumzoa mtu mmoja aliyejikuta akijeruhiwa vibaya na kukimbiziwa hospitali akiwa hoi.

Na Mwandishi Wa Alasiri, Manzese



Gari moja Jijini limekifumua kituo kidogo cha Polisi na kumzoa mtu mmoja aliyejikuta akijeruhiwa vibaya na kukimbiziwa hospitali akiwa hoi.


Aidha, gari hilo limefumua mlingoti wa bendera wa kituo hicho pamoja na zege la kituo baada ya ajali hiyo ya aina yake .


Tukio hilo limetokea Manzese Jijini jana, mishale ya saa 1:00 usiku na kulihusisha gari dogo lenye namba za usajili T 372 AMA.


Taarifa zinasema gari hilo lililokuwa katika mwendo wa kasi, lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyetambuliwa kwa jina la Kamilusi Malulu.


Aidha, mtu aliyezolewa na gari hilo na kujikuta akijeruhiwa vibaya kabla ya kuwahishwa hospitali ametajwa kwa jina la Daudi Sembe, mpita njia aliyekuwa hana hili wala lile wakati akikatiza mbele ya kituo hicho kidogo cha Polisi Manzese.


Wakisimulia mkasa huo, mashuhuda wanasema gari lililosababisha ajali hiyo lilikuwa katika mwendo mkali huku likiyumba hovyo kabla ya kukivaa kituo cha polisi na kuzua kitimtim kwa askari wachache waliokuwa zamu.


`Yaonyesha dereva wa gari hili alikuwa amelewa na kama isingelikuwa kuugonga mlingoti wa bendera na kuzuiwa na ukuta uliojengewa mlingoti huo saa hizi tungesema mengine,` akasema shuhuda mmoja aliyekataa kujitaja jina.


Akafafanua shuhuda huyo kuwa, kama gari hilo lingefika kaunta kulikokuwa na askari na raia kadhaa waliokuwa wakisikilizwa shida zao, ni wazi kwamba wengi wangeumizwa vibaya ama kukatishwa maisha yao.


Baadhi ya askari wa kituo hicho ambao hawakupenda majina yao yatajwe gazetini, wamethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa dereva huyo walimkamata na kisha kumkabidhi kwa watu wa usalama barabarani ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi yake.


`Mungu mwenyewe ndiye aliyetuokoa pale kituoni� jamaa alikuwa akiliendesha kwa kasi na alipokamtwa, alionekana kuwa amelewa na tena akawa na harufu kali ya pombe,` akasema askari mmojawapo.


Hadi mwandishi akiondoka toka katika eneo hilo, tayari polisi walishamdhibiti dereva wa gari hilo aliyekuwa hoi kwa kilevi.


Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents