Gray Mgonja Naye Kortini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, ambaye yuko katika likizo ya kustaafu, Grey Mgonja, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka manane.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, ambaye yuko katika likizo ya kustaafu, Grey Mgonja, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka manane.
Mgonja alisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja wa mahakama hiyo.

Mgonja alisomewa mashitaka hayo na Wakili wa Seriakali Mwandamizi, Fredrick Manyanda, ambaye alidai kuwa Oktoba 10, mwaka 2003, akiwa mtumishi wa umma kama Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alipuuza mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yakimtaka kutoza kodi kwa kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Mgonja kati ya Desemba 18 na 19 mwaka 2003, akiwa mtumishi wa umma na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, aliidhinisha kibali namba GN 423/2003 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Mgonja anadaiwa kuwa katika shitaka la tatu, Desemba 19, mwaka 2003 akiwa mtumishi wa umma na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Manyanda alidai kuwa katika shitaka la nne, Oktoba 15, mwaka 2004 Mgonja akiwa mtumishi wa umma na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alitoa kibali namba GN 497/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tano, mshitakiwa huyo anadaiwa kati Oktoba 14 na 15 mwaka 2004, akiwa mtumishi wa umma na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alitumia madaka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 498/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Katika shitaka la sita, Mgonja anadaiwa kuwa Novemba 15, 2005 akiwa mtumishi wa umma na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 378/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Katika shitaka la saba, Mgonja anadaiwa kuwa Novemba 15, mwaka 2005 akiwa mtumishi wa umma na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 377/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Katika shitaka la nane, Mgonja anadaiwa kuwa kati ya mwaka 2003 na 2007, akiwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo kwa makusudi na kutokuwa makini katika kazi yake, alisaini vibali vya kutoa msamaha wa kodi vilivyotajwa katika mashitaka ya hapo juu ambapo aliisababishia serikali hasara ya Sh.11, 752,350,148.00. Mshitakiwa alikana mashitaka yote.

Upande wa Mashitaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na kwamba hauna pingamizi la dhamana.

Hata hivyo, wakili anayemtetea Mgonja, Profesa Lenard Shaid, aliomba Mahakama kutoa masharti nafuu kwa mteja wake kwa sababu mashitaka yanayomkabili ni yale yanayowakabili mawaziri waandamizi wawili wa zamani Basil Mramba na Daniel Yona katika kesi namba 1200.

Hakimu Mwankenja, alisema kesi hizo ni mbili tofauti, kwa kuwa inayomkabili Mgonja ni kesi namba 1211 na ile ya Mramba na Yona ni namba 1200.

“Kwa sababu mshitakiwa anatuhumiwa peke yake kwa hiyo atajidhamini kwa Sh. bilioni 5.9 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hiyo,“ alisema Hakimu Mwankenja.

Masharti mengine ni kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh. milioni 50 kila mmoja.

Mshitakiwa ametakiwa kuwasilisha mahakamani hati ya kusafiria, kutokutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama.

Mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo na kurudishwa rumande hadi Desemba 29, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.

Mashitaka dhini ya Mgonja yanafanana na yale waliosomewa aliyekuwa Waziri wa Fedha Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba na Waziri wa Nishati na Madini wa awamu hiyo pia, Daniel Yona. Wote wako nje kwa dhamana.

Katika hatua nyingine, viwanja vya mahakama hiyo jana vilifurika askari polisi na gareza zaidi ya 50.

Tangu asubuhi kabla na baada ya ya kufikishwa kwa Mgonja katika Mahakama ya Kisutu, walikuwepo Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) katika eneo la Mahakama wakiwa na mbwa watatu huku wakizunguka huku na kule na kusababisha ulinzi kuwa mkali.

Ilipofika saa 7:20 mchana, Mgonja alifikishwa mahakamani hapo akiwa ndani ya gari aina ya Toyota RAV4 lenye namba za usajili T 123 ATW kisha kusomewa mashitaka saa 8:15.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents