Habari

Hamad Rashid aokoa nyumba yake kunadiwa

KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, Hamad Rashid Mohamed, ameinusuru nyumba yake kupigwa mnada uliopangwa kufanyika kesho kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kushindwa kulipa mkopo wa mamilioni ya fedha

na Happiness Katabazi


KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, Hamad Rashid Mohamed, ameinusuru nyumba yake kupigwa mnada uliopangwa kufanyika kesho kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kushindwa kulipa mkopo wa mamilioni ya fedha alizokopa katika benki moja ya jijini Dar es Salaam.


Hamad ambaye pia ni mbunge wa Wawi kwa tiketi ya CUF, aliweza kunusuru kuuzwa kwa nyumba yake hiyo iliyoko kwenye Kitalu 432, eneo la Kawe, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam baada ya jana alasiri kufanikiwa kulipa kiasi chote cha deni alilotakiwa kukilipa.


Taarifa ambazo Tanzania Daima ilikuwa imezipata kutoka Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara zinaeleza kuwa, Hamad Rashid aliwasilisha fedha hizo mbele ya Jaji Salum Masati ambaye ndiye aliyewaamuru walalamikaji kupokea fedha hizo.


“Ni kweli alasiri hii nimelipa Dola za Marekani 21,055 na fedha nyingine kiasi cha shilingi 6,983,754 ambacho ndicho nilichoelezwa kudaiwa baada ya kukopa kutoka katika benki ya Savings & Finance Commercial Ltd,” alisema Hamad Rashid.


Mbunge huyo ambaye alilazimika kurejea Dar es Salaam na kuacha vikao vya Bunge la Bajeti vikiendelea Dodoma, alisema tangu taarifa za nyumba yake hiyo yenye thamani zaidi ya sh milioni 250 itangazwe kupigwa mnada, baadhi ya watu walishaonyesha dhamira ya kuinyemelea tayari kuinunua hiyo kesho kwa njia ya mnada.


Taarifa nyingine zinaeleza kuwa, hata baada ya kukubali kulipa kiasi hicho cha fedha, Hamad mmoja wa wabunge mashuhuri wa upinzani, amewasilisha nakala ya barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo na Kampuni ya Rhino Auction ambayo ilipewa dhamana ya kuipiga mnada nyumba hiyo akipinga madai yaliyokuwa yakielekezwa dhidi yake.


Aidha, mbunge huyo jana hiyo hiyo alituma taarifa ya maandishi kwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta ambayo gazeti hili limeiona nakala yake, akimtaarifu kuhusu kulipa kiasi hicho cha fedha, sambamba na kueleza malalamiko aliyowasilisha akipinga namna suala zima la mkopo wake lilivyoshughulikiwa katika hali ambayo inatoa mwelekeo wenye utata mkubwa.


Mbunge huyo ambaye alizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, alisema alikuwa akikusudia kudai fidia kubwa kutokana na usumbufu mkubwa aliokabiliana nao kuhusu deni hilo ambalo alisema amekuwa akililipa kwa muda sasa.


Alisema moja ya mambo yanayosababisha afikie uamuzi huo wa kudai fidia, ni ukweli kwamba, benki hiyo imeshindwa kumueleza kwa ufasaha kiasi halisi cha fedha ambacho amekuwa akidaiwa na kila mara amekuwa akipewa kiwango tofauti cha deni, jambo ambalo alisema katika mazingira ya kushangaza hata mahakama ilionekana ikiacha hali hiyo iendelee.


Katika barua yake ya malalamiko, Hamad Rashid alisema hata baada ya kuelezwa kuwa anatakiwa kulipa deni hilo, madai hayo hayakupata kuonyesha kiasi cha dola 3,000 ambacho alipata kukilipa Januari 30, mwaka huu na kiasi kingine cha dola 17,000 alichokilipa katika kipindi cha baada ya Februari 6 na Juni 8, mwaka huu.


Aidha, Hamad anasema pia kwamba, kiasi cha riba kinachofikia sh 10,786,974 alichodaiwa kuwa anapaswa kukilipa hakikuwa sahihi chini ya makubaliano yaliyofikiwa wakati akiomba mkopo wake huo, na kwamba fedha ambazo ndizo zinazodaiwa kuzaa riba hiyo nazo zina utata mkubwa.


Mbunge huyo katika barua yake hiyo, anaeleza kuwapo kwa vitendo visivyozingatia maadili na vya kihalifu, ambavyo vilikuwa vikifanywa kupitia katika akaunti yake, ambavyo navyo amesema anategemea kuvitaja katika malalamiko yake hayo.


Juzi, gazeti moja la kila siku (si Tanzania Daima) liliandika kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, kuamuru kuuzwa kwa mnada kwa nyumba ya mbunge huyo baada ya kushindwa kulipa mkopo wa sh milioni 15 na sehemu ya dola za Marekani 50,000 alizokopa katika benki hiyo ya Saving and Finance Commercial Bank Ltd ya Dar es Salaam.


Katika barua yake aliyomwandikia Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuomba kufanyiwa uchunguzi uhalali wa madai mbalimbali ya benki hiyo dhidi yake, Hamad amekiri kupewa na benki hiyo mkopo wa sh milioni 25 na dola za Marekani 50,000 kwa jina la kampuni yake kwa dhamana ya nyumba yake iliyokuwa kwa Mfilisi wa Benki ya Greenland, Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB).


Hamad alinukuliwa akisema, alichukua mkopo huo kwa ajili ya kugharamia manunuzi ya vyuma chakavu na kuvisafirisha nje ya nchi. Hata hivyo, ameeleza katika deni hilo, alilipa sh milioni 10 kwa wakati na pia sehemu ya dola za Marekani 50,000 alizokopa katika benki hiyo.


Ilidaiwa pia kwamba, uamuzi wa kuuzwa kwa nyumba yake hiyo ulifikiwa baada ya mahakama hiyo katika kesi namba 75 ya mwaka 2006 aliyofunguliwa na benki ambapo mahakama hiyo ilimruhusu dalali wa mahakama, Kampuni ya Rhino Auction Mart Limited, kuiuza nyumba hiyo.


Mahakama hiyo katika maamuzi yake, ilisema mnunuzi atatakiwa kulipa asilimia 25 papo hapo na salio asilimia 75 lilipwe katika muda wa siku 14 kuanzia tarehe ya mnada, vinginevyo atakuwa amepoteza haki zote na mnada utarudiwa.


Kwa mujibu wa gazeti hilo, Hamad alishindwa kulipa mkopo huo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo akaunti aliyochukulia mkopo huo kutotumika tangu Juni 20, mwaka jana.


Sababu nyingine iliyomfanya ashindwe kulipa mkopo huo, anasema inatokana na mteja aliyemuuzia chuma chakavu kutokuwa muaminifu, wakala wa meli, Kampuni ya MAERSK kukataa kutoa nyaraka za kuthibitisha kupokea mzigo na kukubali kuisafirisha (BL) na usimamizi wa biashara zake kuathirika kutokana na kwenda India kwa ajili ya matibabu.


Kutokana na hali hiyo, Hamad alisema chuma hicho chakavu kilipofika India na kukaa muda mrefu bandarini, Mamlaka ya Forodha ya nchi hiyo, ililazimika kukipiga mnada.


“Benki yangu niliiarifu matokeo haya yote na hatua nilizochukua za kuishtaki Kampuni ya MAERSKI kwa kitendo chao cha kukataa kutoa BL, jambo lililosababisha kunadiwa. Katika biashara hii nilipoteza jumla ya dola 150,000. Kesi namba 10/2006 bado iko mahakamani na hadi leo BL ziko mikononi mwao,” alisema.


Awali, nyumba ya Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo iliwahi kupigwa mnada na mahakama baada ya kushindwa kulipa deni alilokopa benki. Pia miaka ya 1990, Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, naye nyumba yake iliwahi kuuzwa kwa mnada, lakini baadaye ikadaiwa kwamba alirejeshewa.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents