Burudani

Hizi ni sababu kwanini vituo vya CNN, Aljazeera, BBC, CCTV au Sky News havina breaking news za Tanzania

Wewe ni miongoni mwa watanzania wengi wanaojiuliza kwanini mashirika makubwa ya habari ya kimataifa yamekuwa yakionesha breaking news za matukio yanayotokea Kenya kuliko vile yanavyofanya kwa Tanzania licha ya kuamini kuwa yapo mambo Bongo yenye uzito yanayostahili kupewa uzito?

breakingnews2

Mfano mzuri ni tukio lililotokea leo nchini Kenya ambapo watu wenye silaha wamevamia chuo kikuu cha Garissa na kuua watu takriban 70 na kujeruhi wengine mamia. CNN, Ajazeera, BBC, CCTV, Sky News na mashirika mengine makubwa ya habari yamekuwa yakirusha live tukio hilo kwenye TV zao na hata mtandaoni.

Tayari #GarissaAttack inatrend kwenye mitandao ya kijamii duniani kote.

Japo haya si mambo ya kufurahia, lakini unaweza kujiuliza tu kwanini matukio kama lile lililotokea juzi ambapo watu wenye silaha walivamia kituo cha polisi katika eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam na kuua polisi wawili na kupora silaha; kwanini halikuweza kupata walau habari ya kawaida CNN au Sky News?

Ni vigezo gani hasa mashirika haya ya kimataifa hutumia kuamua kuzipa uzito habari na kuzicover kwa siku nzima na hata wakati mwingine wiki nzima?

Nimezungumza na waandishi na watangazaji wakongwe na wa kimataifa wawili, Hassan Mhelela wa BBC na Basil Mbakile wa East Africa Radio aliyewahi kuwa mwandishi wa BBC ili watupe ukweli wa mambo.

Mhelela anasema kuna sababu kadhaa kwanini Kenya inamulikwa zaidi na vyombo vya habari vya kimataifa kuliko Tanzania.

“Kenya tayari umeshaona mara nyingi kuna hayo mashambulizi ya kigaidi na tayari Kenya na Alshaaab wana matatizo. Eneo hilo ambalo limetokea hilo tukio la Garissa, wapo hao Alshaabab kwa kiasi kikubwa. Hivyo inategemea na nature ya shambulio, kama ni ujambazi tu haiwezi kuihahalisha kuifanya iwe ni habari ya dunia nzima,” amesema Mhelela.

“Kimsingi ili habari iwe international, inatakiwa kuwe na sababu kuifanya iwe relevant kwa mtazamaji aliyepo Mexico au aliyepo Japan, sababu kama ni mashambulio ya kijambazi kila nchi inayo na huwezi kusema kila tukio la kijambazi ulifanye international story,” ameongeza.

“Ukiangalia matukio ya albino, hayapo nchi nyingine yapo Tanzania na kila yanapotokea Tanzania hivyo vyombo vinacover.”

Basil Mbakile hayupo mbali na Mhelela. Anasema matukio ya kigaidi yameifanya Kenya ivutie ‘attention’ ya mashiriki makubwa ya habari duniani.

“Ugaidi ni sehemu yoyote duniani,” amesema Mbakile. “Ugaidi hauchagui dini wala kabila. Kwa wenzetu wa nchi za Magharibi hasa baada ya yale matukio ya September 11 yaliwagusa sana na ukiangalia mzunguko mzima na mtandao wa ugaidi ulivyo duniani na vikundi vyenye msimamo na itikadi kali za kidini kama kuibuka kwa hili kundi la ISIS ambalo linashikilia maeneo ya Kaskazini mwa Iraq na baadhi ya maeneo ya Syria limekua ni tishio sana kwa nchi za Magharibi, ni mtandao unaoenea kwa kasi,” ameongeza.

“Kuna matukio yanayotokea Tanzania yanaweza kuwa labda mauaji lakini kwa wao kule hawawezi kulichukulia ni tukio zito, wao wataliona kama ni tukio la ndani zaidi linaihusu Tanzania.”

Je! Tanzania haina waandishi wengi wa habari wanaoyafanyia kazi mashirika hayo kiasi cha matukio mengi yanayotokea kwetu kutoyafikia?
Mhelela anadai kuwa wapo wawakilishi wengi wa mashiriki hayo yakiwemo Reuters na mengine.

“Uwepo wa waandishi Tanzania sasa hivi ni mkubwa japokuwa huwezi kulinganisha na Kenya sababu Kenya ni ‘hub’ ya mashirikia mengi ya kimataifa. Equally unaweza ukasema kwanini habari za teknolojia zinatokea Kenya zaidi kuliko Tanzania? Jibu linaweza kuwa kwamba mashirika mengi yana ofisi zao za kanda Nairobi; kwa mfano akina Facebook, Microsoft, Google kwahiyo huwezi kushindanisha na yanayotokea Tanzania.”

Mhelela ameongeza kuwa utulivu na amani iliyopo Tanzania imeyafanya mashirika hayo yasiitupie zaidi macho nchi hii na kuyaona matukio yanayoonekana makubwa nchini, madogo mno kwao.

“Unakuta hata uchaguzi wa Tanzania hauna interest kwa vyombo vingine kwasababu uko hivyo lakini ukifuatilia uchaguzi unapofanyika Kenya kwa mfano unakuta ni heka heka kubwa,” amesisitiza.

“Unaweza kusema juzi askari waliuawa pale Mbagala, lakini je tunafahamu kwamba ilikuwa ni ugaidi au ulikuwa tu ni ujambazi wa kuiba silaha ili waende wakafanyie uhalifu? Lakini juzi juzi hapa kulikuwa na lile tukio la Emwazi yule Jihad John, katika vyombo ambavyo waliifuatilia kwa kina ile story, vilikuwa ni vyombo vya nje, vyombo vya ndani wala havikuipa umuhimu ile story. Labda watu waliona pengine ni tukio la zamani lakini wenzetu wakaingia kwa undani zaidi wakachimba kwamba alikuja kufanya nini.”

Naye Mbakile amegusia jinsi ambavyo matukio ya mauaji ya albino yanavyomulikwa na vyombo hivyo.

“Mpaka Daily Mail ya Uingereza waliandika kwa kirefu sana, News24 ya Afrika Kusini wameandika hiyo habari kwa kirefu. Juzi migongano kati ya Kardinali Pengo na Gwajima ingawa sio kwa kiwango hicho kwamba useme kwamba Aljazeera wataandika, CNN watacover, hapana. Lakini kwa BBC wanaweza wakaichukua kwasababu inagusa eneo ambapo wao wana wasikilizaji na watazamaji wao eneo la Afrika Mashariki.”

Hata hivyo Mhelela anasema mitandao ya kijamii inaweza kuiweka pia Tanzania kwenye jicho la vyombo vya habari vya kimataifa japo anadai lugha inayotumika inaweza kuwa ni kikwazo pia.

“Ukipost kwa Kiswahili, haisafiri kwa umbali sana story yako lakini ikiwekwa kwa Kiingereza mathalan, inaweza kuwa ni story ndogo leo lakini kesho ikaonwa na mtu yupo Canada, akaifuatilia akataka kuipa angle tofauti.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents