Habari

‘Jambazi’ ajikabidhi kwa waziri bungeni

JUMANNE Ally Mjusi, aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba na Jeshi la Polisi mkoani humu kwa tuhuma za kuhusika katika matukio kadhaa ya ujambazi, amejisalimisha bungeni mjini Dodoma.

na Mustafa Leu na David Frank, Arusha


JUMANNE Ally Mjusi, aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba na Jeshi la Polisi mkoani humu kwa tuhuma za kuhusika katika matukio kadhaa ya ujambazi, amejisalimisha bungeni mjini Dodoma. Kamanda Polisi Mkoa wa Arusha, Basilio Matei, alisema kuwa mtuhumiwa huyo alijisalimisha juzi mjini Dodoma, kwa Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohammed Aboud.


Akisimulia mkasa wa kujisalimisha kwa mtuhumiwa huyo, Kamanda Matei alisema kuwa, alipoingia katika Ukumbi wa Bunge kwa nia ya kumuona naibu waziri huyo, Mjusi alionana kwanza na wasaidizi wake.


Alisema kuwa Mjusi aliwaambia wasaidizi wa naibu waziri kuwa, alikuwa anatuhumiwa kwa ujambazi kwa uonevu, na hivyo ameamua kuonana na Aboud ili kujisalimisha kwani alisikia kuwa anatafutwa.


Mbali ya ya hilo, Kamanda Matei alieleza kuwa, wasaidizi wa waziri walipowasiliana naye, aliwaagiza waendelee kumshikilia wakati taratibu za kumrejesha Arusha zikifanywa.


“Ni kweli tumemshikilia mtuhumiwa wetu, nilipigiwa simu na wasaidizi wa naibu waziri kutokea bungeni, ambako alienda kujisalimisha… walinieleza kuwa walikuwa wanamshikilia mtuhumiwa huyo aliyekuwa akisakwa kwa tuhuma mbalimbali,” alisema.


Kamanda Matei alisema kuwa tayari wameshatuma kikosi maalum pamoja na gari kwenda kumchukua mtuhumiwa huyo mjini Dodoma ili arejeshwe Arusha anakokabiliwa na tuhuma kadhaa za ujambazi.


Pamoja na mambo mengine, inadaiwa kuwa, wiki mbili zilizopita, Mjusi akiwa na wenzake wawili, akiwamo mtoto wake wa kufikia, walivamia hospitali binafsi ya Ithinashir ya mjini hapa na kupora sh milioni 17 ambazo zilikuwa ni mishahara ya watumishi wa hospitali hiyo.


Katika tukio hilo, watu wawili, akiwemo mtoto wake Mjusi, walikamatwa na walimtaja Mjusi kuwa ndiye kiongozi wao, wakimhusisha na umilikaji wa silaha mbalimbali, zikiwamo SMG na bastola ambazo amekuwa akizitumia katika matukio ya ujambazi.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents