Habari

Jihadharini na matapeli, Mramba awaambia wananchi

Serikali imesema ina imani kuwa sehemu kubwa ya ajali za moto na za barabarani zinasababishwa na `majini.`, akimaanisha bidhaa feki za kitapeli.

Na Simon Mhina

 
Serikali imesema ina imani kuwa sehemu kubwa ya ajali za moto na za barabarani zinasababishwa na `majini.`, akimaanisha bidhaa feki za kitapeli.

 

Mheshimiwa Basil Mramba, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko amesema Serikali imepata tetesi juu ya “majini” na mazingira ambayo kwa muda mrefu sasa ni chanzo cha matukio ya ajali hizo.

 

`Jamani kama kuna jini basi jini hilo linatokea China, linakuja kwenye kontena na meli-Nasema kama kuna jini linalounguza nyumba basi ni nyaya feki na vyombo feki vya umeme ambavyo tayari tumevikamata bandarini vikitokea China, `akasema Bw. Mramba.

 

Akasema baada ya kufuatilia matukio mbali mbali yaliyohusisha nyumba za watu kuteketea kwa moto, Serikali imebaini kuwa tatizo sio la Tanesco wala majini kama baadhi ya watu wanavyodhani, bali ni nyaya, swichi na soketi feki wanazofunga majumbani mwao.

 

Huku akionyesha vifaa hivyo, Waziri Mramba akasema sura na kwa rangi ya vifaa hivyo feki, vinafanana kopi raiti na ya vifaa kama hivyo vinavyotengenezwa nchini.

 

Akasema tofauti iliyopo ni kwamba waya hizo hazielezi jina la mtengenezaji wala anwani yake.

 

`Huu ni utapeli kabisa, hakuna mtu anayetengeneza bidhaa aache kujitaja,` akasema.

 

Bw. Mramba akaonya kwamba Watanzania wengi wataendelea kulizwa na kupata hasara katika jambo hilo, kwa tabia yao ya kuendekeza vya bwerere.

 

Akasema vifaa feki toka China, India na Dubei, huuzwa kwa bei chee hali inayowafanya watu wavipapatikie.

 

`Jamani waambieni Watanzania wanatapeliwa, wanaumizwa, wasifurahie kununua bidhaa feki eti kwa vile ni bei rahisi,` akaonya.

 

Waziri Mramba akasema kwamba kutokana na nyaya hizo kuwa feki, haziwezi kustahimili umeme wa Tanzania, hali inayopelekea kushika moto na kulipuka.

 

Kuhusu matairi, waziri Mramba akasema `Kama kuna majini ya ajali huko barabarani, basi jini hilo ni matairi feki toka Dubai`.

 

Akasema kama ilivyo kwenye nyanya, wenye magari pia huponzwa na bei chee ya matairi hayo.

 

Akasema matajiri wengi wenye magari hasa ya biashara, wanaona ni ujanja sana kununua tairi hizo, ambazo hazina ubora unaokidhi haja.

 

`Kwanini ajali zisitokee wakati kwenye magari watu wanafunga matairi ya ovyo `akahoji.

 

Bw. Mramba amewaomba watanzania kushirikiana na serikali wakati huu ambapo wameamua kuvalia njuga tatizo hilo.

 

Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents