Kenya: Raila Odinga anza kuonja matunda ya Uwaziri Mkuu

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), nchini Kenya, Raila Odinga, ameanza kupewa ulinzi wa serikali, ikiwa ni hatua ya kwanza muhimu ya kutambua nafasi yake mpya ya kuwa Waziri Mkuu.

Na Mwandishi Wa Mwananchi

 

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), nchini Kenya, Raila Odinga, ameanza kupewa ulinzi wa serikali, ikiwa ni hatua ya kwanza muhimu ya kutambua nafasi yake mpya ya kuwa Waziri Mkuu.

 

 

 

Nafasi hiyo ya Waziri Mkuu inayotarajiwa kupitishwa rasmi na Bunge la nchi hiyo kesho, ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya pande mbili zilizokuwa zikipingana tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Desemba 27, mwaka jana kukubali kutia saini mkataba wa serikali ya umoja wa kitaifa.

 

 

 

Taarifa zilizopatikana kutoka kwenye vyanzo vya serikali jijini Nairobi jana zilieleza kuwa Raila alipatiwa ulinzi rasmi kwa saa 24 tangu juzi ikiwa ni pamoja na usafiri rasmi wa kiofisi na dereva maalumu.

 

 

 

Hiyo ni sehemu ya maandalizi ya makubaliano ya kurejesha cheo cha uwaziri mkuu na kumfanya Raila Odinga kuwa Waziri Mkuu wa pili tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1964.

 

 

 

Kwa mara ya kwanza nafasi hiyo ilishikwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, hayati Jommo Kenyatta mwaka 1963; ambaye alifuta cheo hicho mwaka 1964 baada ya kupata Uhuru kamili na yeye kuwa Rais na Mtendaji Mkuu wa Serikali.

 

 

 

Raila alianza kuonja matunda hayo muda mfupi kabla ya kukutana rasmi na Kibaki kujadiliana juu ya mgawanyo wa nafasi muhimu katika Baraza la Mawaziri kabla ya Bunge la nchi hiyo kukaa kesho.

 

 

 

Gazeti la The Nation la nchini Kenya, lilisema jana kuwa mara baada ya kutoka katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa saa mbili kwenye ofisi za Rais zilizopo kwenye Jengo la Harambee, Odinga alisema chama chake na PNU vitakubaliana kuhusu mgawanyo wa nafasi za mawaziri baada ya kupitishwa muswada wa serikali ya umoja kesho.

 

 

 

Alisema kikao maalumu cha wabunge kitafanyika kesho asubuhi na kufikia muafaka juu ya namna muswada huo utakavyopitishwa na kuanza utekelezaji, kabla ya Rais Kibaki kufungua rasmi kikao cha Bunge kwa ajili ya kupitishwa muswada huo mchana.

 

 

 

Hata hivyo, maafisa wa kikosi maalumu cha ulinzi na huduma kwa viongozi walisema kutokana na umuhimu wa nafasi hiyo pia ulinzi umeelekezwa nyumbani kwa Raila kwenye mji wa Bondo, ili kuimarisha usalama wakati makazi mapya ya Waziri Mkuu yakiandaliwa haraka.

 

 

 

Utaratibu huo ulibainika mapema baada ya kikao maalum cha maafisa watendaji wakuu wa Ofisi ya Rais na serikali juzi, ambao pia waliandaa magari manne ya kifahari aina ya Limousines kwa ajili ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo anayetarajiwa kuthibitishwa mara baada ya kupitishwa kwa muswada unaothibitisha nafasi hiyo kwenye Bunge la nchi hiyo kesho.

 

 

 

Walisema baada ya kukamilisha suala hilo muhimu la kuweka utaratibu maalumu wa ulinzi kwa Raila, hatua inayofuata ni kwa maafisa wa serikali kuandaa makazi na ofisi mpya kwa ajili ya Waziri Mkuu mpya.

 

 

 

Vyanzo vya ndani ya serikali vilikaririwa na gazeti la The Standard jana kuwa, kwa sasa suala la makazi na ofisi ya Waziri Mkuu linapewa kipaumbele. Makazi maalumu ya Waziri Mkuu yatakuwa nje ya Ikulu ya nchi hiyo.

 

 

 

Kufuatia makubaliano hayo yaliyofikiwa chini ya usimamizi wa Msuluhishi wa Kimataifa wa mgogoro huo, Kofi Annan, Raila atakuwa kiongozi wa pili mwenye mamlaka nchini humo baada ya Rais Kibaki.

 

 

 

Hatua hiyo ya nafasi na madaraka anayotarajia kupewa Raila imeendeleza kuzua maswali kadhaa kwa baadhi ya Wakenya, kwa kuwa madaraka hayo yanaweza kumfanya kuwa mtu mwenye madaraka makubwa baada ya Rais.

 

 

 

Wakenya wanaendelea kuangalia utekelezaji wa makubaliano hayo, wengi wao wakielekeza macho yao kwa viongozi hao wawili ambao huenda wakachangia ofisi zilizopo kwenye Jengo la Harambee.

 

 

 

Makubaliano ya kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa yalifikiwa mwishoni mwa wiki iliyopita ili kumaliza mgogoro na vurugu zilizotokea nchini humo mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Desemba 27, mwaka jana zilizosababisha zaidi ya watu 100 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 500,000 kukimbia makazi yao.

 

 

 

Imeandaliwa na Andrew Msechu kwa msaada wa Mashirika ya Habari

 

 

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents