Habari

Kesi ya Chitalilo yaiva

MBUNGE wa Buchosa, Samwel Chitalilo (CCM), anayetuhumiwa kughushi vyeti na kudanganya kuhusu elimu yake, atapanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza Mei 14

na Happiness Katabazi


MBUNGE wa Buchosa, Samwel Chitalilo (CCM), anayetuhumiwa kughushi vyeti na kudanganya kuhusu elimu yake, atapanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza Mei 14, mwaka huu ambapo maombi ya kutaka ashitakiwe kwa utaratibu binafsi (private prosecution) yatatajwa kwa mara ya kwanza.



Kwa mujibu wa mlalamikaji wa kwanza, Alfred Ngotezi, suala hilo limesajiliwa kwa namba 1 ya mwaka 2007 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza.



Wiki mbili zilizopita, waombaji waliwakilisha ombi lao Mahakama Kuu Mwanza, hata hivyo wanasheria wao walilihamishia Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza kwa kuwa masuala yote ya jinai huanzia huko kabla ya kufikishwa Mahakama Kuu.



Ombi hilo tayari limepangwa kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi, Mushi, wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mwanza, Mei 14, mwaka huu.



Mbunge huyo alikaririwa na gazeti hili Machi 6 kuwa, ataendelea kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 20 ijayo pamoja na polisi kuthibitisha tuhuma zake za kughushi vyeti.



Aprili 11 mwaka huu, Ngotezi ambaye ndiye aliyefungua jalada namba SEN/104/2006 la uchunguzi kuhusu elimu ya Chitalilo, mjini Sengerema mkoani Mwanza mapema mwaka jana na mpiga kura mwenzie wa Buchosa, Henriko Msheleja, walipeleka maombi Mahakama Kuu mjini Mwanza wakiomba waruhusiwe kumshtaki Chitalilo kwa utaratibu wa uendeshaji mashtaka binafsi chini ya kifungu cha 99 cha mwenendo wa makosa ya jinai.



Katikati ya Machi mwaka huu, Msheleja alifika katika ofisi za gazeti hili, akiwa na mpiga kura mwenzake, Radhamani Amani, wakiwa na majina na saini za wapiga kura wengine 184 wa jimbo hilo, wakiomba msaada wa kisheria ili kumshtaki Chitalilo kwa kudanganya kuhusu elimu yake.



Hatua hiyo ilitokana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba kulithibitisha Tanzania Daima Machi 4 mwaka kuwa, mbunge huyo alikuwa amedanganya kuhusu elimu yake katika uchaguzi wa 2000 na 2005, lakini akasema polisi haiwezi kumfungulia mashtaka kwa sababu hakuwa amevunja sheria ya uchaguzi.



Kwa kawaida, masuala yote ya jinai hushughulikiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), isipokuwa pale inapobidi kufanya kinyume, ambapo ruhusa maalum inaweza kutolewa na Mahakama Kuu kwa kutumia kifungu cha 99 cha mwenendo wa makosa ya jinai.



Hati ya mashitaka inaeleza kuwa, Chitalilo alidanganya wapiga kura kwa kutoa vipeperushi, akionyesha kuwa alimaliza kidato cha nne kwenye Shule ya Sekondari ya Bupandagila mkoani Shinyanga kati ya 1985 hadi 1990 na kuwa alisoma Sekondari ya Katikamu nchini Uganda kati ya 1990 na 1991.



Walalamikaji wanadai pia katika hati hiyo kuwa, Baraza la Mitihani la Uganda na Shule ya Katikamu, wametoa nyaraka kukanusha kuwa Chitalilo aliwahi kusoma huko.



Wanadai pia kuwa, wamewasilisha malalamiko yao katika ngazi mbambali za utawala, bila mafanikio yoyote.



Kwamba mbunge huyo alikula kiapo cha uongo kwa kujaza sifa zisizokuwa za kweli kwenye nyaraka za serikali mbele ya ofisa mwenye dhamana.



Wameongeza kuwa, pindi polisi walipoanza kuchuguza elimu yake, alibadilisha wasifu aliokuwa ameweka kwenye tovuti ya Bunge, mabadiliko ambayo hata hivyo wanadai yanaonyesha kuwa alimaliza kidato cha pili kwenye Sekondari ya Bupandagila mwaka 1991 ilhali akiingia kidato cha tano mwaka huo huo wa 1991


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents