Michezo

Kilimanjaro Marathon 2016 yazinduliwa Moshi

Mbio za Kilimanjaro Marathon 2016 zimezinduliwa Mjini Moshi huku ikiwa imebaki takriban mwezi mmoja kabla yam bio hizo kufanyika.

P1850442 GROUP PHOTO
Wadhamini wa Kilimanjaro Marathon 2016 wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga na viongozi wengine wakati wa uzinduzi wa mbio hizo Mjini Moshi

Uzinduzi huo ulifanyika Kibo Palace Homes Mjini Moshi na kuhudhuriwa na wadadhamini wa mbio hizo na wadau mbalimbali wa riadha kuonesha ukubwa wa tukio hilo.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikuli, Meneja wa Mauzo wa TBL Kilimanjaro na Tanga, Richard Temba alisema mbio hizo zitafanyika Februari 28, 2016 wilayani Moshi na zitahusisha wanariadha wa ndani na nje ya nchi kutoka pande mbalimbali za dunia.

“Tumeonelea ni vizuri kuzindua mbia hizi rasmi hapa Moshi ambako zitafanyika ili kuashiria kuwa mambo yameiva,” alisema.

“Kilimanjaro Premium Lager imeingia mwaka wake wa 14 kama mdhamini mkuu wa mbio hizi, kwa mafanikio makubwa na kuyafanya kuwa moja ya mbio kubwa zaidi za marathon barani Afrika, kwani kwa sasa hujumuisha zaidi ya wanariadha 7,000 kutoka nchi zaidi ya 45 kote duniani,” alisema Temba.

Alisema Kilimanjaro Premium Lager imewekeza zaidi ya shilingi milioni 500 katika mashindano haya na kuwa hapo baadaye watatangaza mchanganuo mzima wa zawadi zitakazotolewa.

Alitoa shukurani za pekee kwa Mkoa wa Kilimanjaro na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) zamani kikiitwa MUCCoBS kwa kuwa wenyeji wa mashindano hayo.

Akizindua mbio hizo Mjini hapa, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga aliwapongeza Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wengine na waandaaji kwa kujielekeza vyema kila mwaka, akiongeza kuwa mashindano yametokea kuwa moja ya matukio makubwa zaidi ya kimichezo ndani na nje ya nchi.

“Mashindano haya pia yamekwenda mbali zaidi katika kukuza utalii kwani wanariadha wa kimataifa na wageni wao hufanya utalii baada ya mashindano na hiyo kufaidisha uchumi wa nchi,” alisema huku akisisitiza kuwa mbio hizo zitatoa fursa nyingi sana hasa za kibiashara.

Aliwataka wanariadha wa Tanzania kuhakikisha wanajiandaa vyema ili watwae zawadi nyingi zaidi kwa kadiri zilivyopangwa kwa kila mbio. Aliongeza kwamba wizara yake inaunga mkono kabisa ubunifu kama huo na kuzitaka kampuni nyingine kufuata nyayo hizo kwa kudhamini mashindano hayo ya kila mwaka.

Aliwapongeza waandaaji, Wild Frontiers, waratibu wa kitaifa-Executive Solutions, Chama cha Riadha Tanzania (RT) na wizara yenye dhamana ya michezo kwa kuhakikisha siku zote kwamba tukio hili linafanikiwa.

“Mbio hizi zimeleta mwamko mpya katika riadha hapa nchini kwa kuwapa fursa vijana wetu wanaochipukia kuweza kujipima na wanariadha mashuhuri kimataifa. Changamoto hii imekuwa na faida kubwa ambapo vijana wetu wameweza kutambua uwezo wao na kuweza kujiamini zaidi wanapoenda kushiriki mashindano mbalimbali kwenye nchi za kigeni,” alisema.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents