Habari

Lowassa aomba wataalamu

WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, ameiomba serikali ya New Zealand, kutuma nchini mabingwa wa elimu na madini pamoja na wa utengenezaji wa mafuta ya petroli kwa kutumia mazao.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima

 

WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, ameiomba serikali ya New Zealand, kutuma nchini mabingwa wa elimu na madini pamoja na wa utengenezaji wa mafuta ya petroli kwa kutumia mazao.
Lowassa, ambaye yuko hapa kwa mkutano wa Umoja wa Serikali za Mitaa wa Jumuiya ya Madola, alitoa ombi hilo katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa New Zealand, Helen Clark, akisema kuwa mpango huo utakuwa ni sehemu ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Alisema kwa vile kuwafundishia Watanzania New Zealand ni gharama kubwa, nchi hiyo inaweza kutuma mabingwa wake nchini na kuweza kuwafundisha watu wengi kwa wakati mmoja.
New Zealand ina ujuzi na uzoefu mkubwa katika maeneo ya elimu, madini, utengenezaji mafuta kwa kutumia mazao, kilimo na mifugo.
Imekuwa ikitoa nafasi chache za masomo kwa Tanzania na misaada ya kiufundi na kiuchumi ambayo New Zealand imo katika mfumo wa misaada inayotolewa na nchi mbalimbali kwa pamoja.
Vile vile, New Zealand, ambayo ni nchi ya Mashariki ya Mbali, husaidia mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali nchini Tanzania.
Mazungumzo ya Lowassa na Clark, yaliyofanyika Ikulu, yalihusu uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili na hali ya kisiasa Afrika.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa New Zealand alisema nchi yake inafanya mapitio ya mkakati wake wa utoaji misaada kuona uwezekano wa kuongeza misaada zaidi kwa Afrika.
Aliipongeza Tanzania kwa msimamo wake katika medani za kimataifa, hasa jinsi ilivyoiunga mkono New Zealand katika uteuzi wa wagombea wa nchi hiyo katika nafasi za Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola na Jaji wa Mahakama Kuu ya Kimataifa.
Raia wa New Zealand, Donald Mckinnon, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola katika mkutano mkuu wa Jumuiya hiyo mwaka 1999 na Sir Kenneth James Keith, alichaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Novemba 2005 kuwa Jaji katika Mahakama hiyo ya kimataifa.
Leo, Lowassa atauhutubia mkutano wa Umoja wa Serikali za Mitaa wa Jumuiya ya Madola, akiwa ni mmoja wa viongozi wazungumzaji wakuu katika mkutano huo.
Sherehe za ufunguzi wa mkutano huo zilifanyika jana alasiri katika ukumbi wa kituo cha Aotea Centre mjini hapa, ambako mkutano huo unafanyika.
Lowassa, ambaye ujumbe wake uliwasili mjini hapa Jumapili, jana alipokewa rasmi katika sherehe iliyojumuisha kukagua gwaride na mapokezi ya kimila ya kabila la Wamaori, ambao ndiyo wenyeji wa visiwa vya New Zealand kabla ya kufika Wazungu kutoka Ulaya.
Jana usiku, Lowassa alitarajiwa kuhudhuria karamu ya chakula cha usiku, iliyoandaliwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Clark kwenye hoteli ya Langham alikofikia.
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents