Habari

Madereva mabasi Tanzania kuanzia miaka 34

UMRI wa madereva watakaruhusiwa kuendesha magari ya abiria unaweza kupandishwa hadi miaka 34, endapo wadau wa usafiri wa majini na nchi kavu watakubaliana na mapendekezo yanayoanza kujadiliwa jijini Dar es Salaam leo.

Na Leon Bahati

UMRI wa madereva watakaruhusiwa kuendesha magari ya abiria unaweza kupandishwa hadi miaka 34, endapo wadau wa usafiri wa majini na nchi kavu watakubaliana na mapendekezo yanayoanza kujadiliwa jijini Dar es Salaam leo.

 

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), madereva hao wa mabasi ya abiria, zikiwamo daladala, watalazimika kuwa wamesoma na kupata cheti cha mafunzo ya udereva kutoka katika chuo kinachotambuliwa.

 

Mapendekezo hayo yanatolewa kukiwa na malalamiko miongoni mwa watumiaji wa huduma ya daladala jijini Dar es Salaam na miji mbalimbali Tanzania kuhusiana na umri mdogo wa madereav wa magari hayo.

 

Mara kadhaa, abiria wamekuwa wakilalamika kuwa vijana wenye umri usizodi miaka 20, wamekuwa wakiendesha daladala kwa fujo na hivyo kuhatarisha maisha ya mamilioni ya watumiaji wa huduma hiyo.

Katika mapendekezo yake, Sumatra pia wanataka abiria wanaosafiri na mabasi kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kufunga mikanda wakati wote na daladala zote zitatakiwa kuwa na milango miwili, mmoja ukiwa ni wa dharura.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya Sumatra, wamiliki wa mabasi ya abiria watatakiwa pia kuhakikisha kuwa magari yao yanafanyiwa ukaguzi na matengenezo ya mara kwa mara kutoka katika gereji yenye usajili.

Ndani ya mapendekezo hayo inaelekeza kuwa mabasi hayo yatazingatia viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuepuka matatizo yanayosababishwa na muundo wa mabasi ya abiria unaotumia mabati hafifu yanayosababisha kuharibika vibaya inapotokea ajali.

Vile vile mabasi hayo yatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuepukana na tatizo la viti vyenye nafasi finyu na kusababisha abiria kukaa kwa taabu na mengine kulazimisha kuwa na safu tano za viti.

Mapendekezo hayo yamedhamiria kuhakikisha kasoro hizo zinaondolewa na kuhakikisha mabasi yote yanatengenezwa kulingana na mapendekezo ya utafiti uliofanywa na kuthibitishwa TBS.

Watakachotakiwa kufanya leo wadau wa Sumatra ni kujadili na kutoa maoni yao yatakayoboresha mapendekezo hayo kabla ya kukabidhiwa kwa serikali ili yatengenezewe muswada ambao baada ya kupewa baraka za Bunge, utatungiwa sheria kamili zitakazosimamia vyombo vya usafiri wa abiria nchini.

 

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa Sheria za Usafiri Barabarani, Anastas Selemani, alisema lengo la mjadala wa leo ni kuyaboresha mapendekezo ya Sumatra ili kuweka mfumo mzuri wenye ufanisi katika sekta ya huduma za usafiri wa abiria nchini.

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents