Mafisadi wamtesa Sitta

JINAMIZI la tuhuma za ufisadi zilizosambazwa katika mtandao wa intaneti zikimlenga Spika wa Bunge, Samuel Sitta, sasa zinaonekana kuvuka mpaka na kuanza kuigusa na kuisumbua familia yake

na Salehe Mohamed na Rahel Chizoza, Dodoma




JINAMIZI la tuhuma za ufisadi zilizosambazwa katika mtandao wa intaneti zikimlenga Spika wa Bunge, Samuel Sitta, sasa zinaonekana kuvuka mpaka na kuanza kuigusa na kuisumbua familia yake.

Akizungumza bungeni jana asubuhi mara tu baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Sitta alisema kundi la watu ambalo hakulitaja, limefikia hatua ya kumtumia mtoto wake mmoja aliyeolewa ujumbe wa maneno machafu ambayo hata hivyo hakutaka kuuweka bayana.

Sitta ambaye anatoa majibu hayo yeye mwenyewe moja kwa moja au kupitia Ofisi ya Bunge kwa mara ya nne sasa, aliwataka wale wanaomtuhumu yeye kuacha kuwahusisha watoto wake katika harakati zao hizo, na badala yake kumlenga yeye aliye na uwezo wa kuwakabili.

Huku akionyesha kuwafahamu watu wanaomtuhumu, Sitta alisema harakati zao hizo hazitamfanya atetereke katika harakati alizozianzisha za kuleta mabadiliko katika shughuli za Bunge.

Hata hivyo, katika majibu hayo, yaliyoonyesha wazi kuwalenga watu fulani ambao Spika hakuwataja kwa majina, aliwataka wamsakame yeye na kuwaacha watoto wake ambao hawana uwezo wa kukabiliana nao.

Kauli hiyo ya Sitta, kimantiki inafanana na ile iliyotolewa na Ofisi ya Bunge hivi karibuni, ikimtetea dhidi ya tuhuma na ikaonyesha wazi wazi kuwalenga wale walio nyuma ya mambo hayo na matukio ya hivi karibuni ya ufisadi wa Richmond, EPA na mabadiliko anayoyafanya ndani ya Bunge.

“Nawaambia wale ndugu zangu wenye kutumia siasa za chini na chafu wasielekeze mashambulizi kwa watoto wangu, kwani hawajawakosea kitu, kama kukosea ni mimi, hivyo ni vema wakanishambulia mimi ambaye nina ubavu wa kuyakabili mashambulizi,” alisema Sitta katika kauli inayofanana na ile aliyoitoa bungeni mwaka jana, Nazir Karamagi.

Mwaka jana wakati wa tuhuma za Karamagi kusaini mkataba wenye utata wa Buzwagi wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini, alipata kuliambia Bunge kuwa, suala hilo lilianza kuwaletea matatizo hata watoto wake ambao walikuwa wakisumbuliwa na wenzao shuleni.

Akifafanua huku akionyesha masikitiko makubwa, Sitta alisema kuwa, hivi karibuni, binti yake ambaye ameolewa alitumiwa ujumbe wenye maneno machafu.

Kwa kuonyesha dharau dhidi ya watu wanaolenga kumchafua, Sitta alizitaja harakati za watu hao kuwa ni ‘siasa za majitaka’ na kusema kuwa amejizatiti kukabiliana nazo.

Katika harakati za kukabiliana na mashambulizi hayo mabaya, Sitta alisema tayari ameshamwagiza Katibu wa Bunge, kuandaa orodha ya malipo yote yaliyotolewa kwake (Sitta) tangu aliposhika wadhifa huo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka 2005 hadi hivi sasa.

Alisema kuwa orodha hiyo inalenga kujibu tuhuma zilizolenga masuala rasmi ambayo yanamhusu yeye katika wadhifa wake wa Spika na wala hatojihangaisha kujibu kashfa zinazohusiana na masuala aliyoyaita kuwa ni ya kijamii.

Sitta alisema kuwa hasumbuliwi sana na siasa hizo za majitaka na kuwa yupo tayari kujibu kila tuhuma inayohusu utendaji wake.

“Nimeongea na wasaidizi wangu na nimewaambia watayarishe taarifa ya malipo ya fedha nilizozitumia tangu nilipochaguliwa hadi hivi sasa na kabla ya kumaliza mkutano huu nitazigawa kwa kila mbunge,” alisema Sitta.

Alisema taarifa hiyo haitahusisha matumizi binafsi, bali ni yale ya ofisi ambayo yamekuwa yakiandikwa na vyombo vya habari kuwa ametumia vibaya.

Akifafanua kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ubadhirifu wa fedha anaodaiwa kuufanya, Sitta alisema kwa taratibu za Bunge, Spika hapewi fedha bali wasaidizi wake ndiyo ambao husimamia kila kitu, hivyo kuhusishwa kwake na ufujaji wa fedha ni mbinu za kumchafulia jina lake.

“Hizi hujuma hazina msingi kwani mimi sipewi fedha mkononi, bali wasaidizi wangu ndiyo hufanya kila kitu, sasa nashangaa kwa nini hao watu hata hawajui taratibu za Bunge na kuamua kunituhumu kufuja fedha,” alisema Sitta.

Aidha, alisema kama watu hao wana lengo la kumdhoofisha ili asiweze kufanya shughuli zake za Bunge vizuri, basi wamekosea kwani ataendelea kuchapa kazi kama kawaida yake.

Kauli hiyo ya Sitta imekuja siku chache baada ya kuibuka kwa taarifa zinazomhusisha na ubadhirifu wa fedha za umma na kashfa nyingine kadhaa kuhusu hayo aliyoyaita masuala ya jamii.

Kabla ya kutoa ufafanuzi huo jana, hivi karibuni, Ofisi ya Bunge ilisambaza tangazo katika vyombo mbalimbali vya habari, ikikanusha habari iliyoandikwa na gazeti hili kuhusu tuhuma hizo dhidi ya Sitta.

Habari iliyokanushwa na Ofisi ya Bunge iliandikwa kutokana na mahojiano ambayo Tanzania Daima iliyafanya na Katibu wa Bunge Damian Foka kuhusu tuhuma hizo dhidi ys Sitta, ambazo zilikuwa zikimhusisha na matumizi mabaya ya fedha za Bunge ikiwa ni pamoja na madaraka yake ya u-Spika.

Foka katika mahojiano hayo na Tanzania Daima alikiri madai yaliyoandikwa katika mtandao wa intaneti yanayoeleza kuwa, Sitta aliwasilisha risiti ya shilingi milioni mbili aliyonunulia dawa kutoka katika duka moja la dawa lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Aidha alisema baada ya kuwasilisha risiti hiyo, alimwelekeza alete pia cheti cha daktari kilichokuwa kikionyesha kuwa alitakiwa kutumia dawa zenye gharama hizo kutokana na matatizo yake ya kiafya katika kipindi cha wiki moja.

“Ni kweli kuwa Sitta alilipwa shilingi milioni mbili katika kipindi cha wiki moja kwa ajili ya kununulia dawa katika duka la dawa la Oysterbay,” alisema Foka katika mahojiano hayo.

Alisema malipo hayo ni halali kwa sababu Ofisi ya Bunge ina taarifa kuhusu matatizo ya kiafya ya Spika Sitta, ambayo hata hivyo hakutaka kuyaweka bayana kwa madai kuwa maradhi ya mtu ni siri yake na daktari wake.

Hata hivyo taarifa ambazo gazeti hili linazo zinaeleza kuwa, Spika amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya miguu ambayo kimsingi ndiyo aliyokuwa akiyatibu kupitia dawa alizonunua katika duka hilo la dawa.

Jana kabla ya kuahirisha Bunge alasiri, Sitta alilieleza Bunge kwamba, tatizo lake la mguu lilikuwa limepata tiba na alikuwa tayari kushiriki katika mazoezi ya timu ya Bunge.

Kuhusu madai kwamba Spika amekuwa akijihusisha katika matumizi mabaya yasiyotambulika kisheria na kikanuni kwa madaraka yake ya magari mawili ya Bunge aliyopewa kwa shughuli zake binafsi, Foka alilieleza Tanzania Daima wakati huo kuwa, hakuwa na taarifa hizo na kuongeza kuwa uwezekano wa kuwepo kwa jambo hilo ni mdogo.

Wakati Foka akitoa taarifa hizo, maofisa kadhaa wa Bunge waliozungumza na Tanzania Daima siku hiyo hiyo, walieleza kuwa, siku chache zilizopita ofisi ya Katibu wa Bunge ilipata kumhoji Sitta kuhusu kuwapo kwa madai hayo yanayomhusisha na matumizi yasiyofaa ya magari ya umma.

Mahojiano kati ya Foka na gazeti hili yalifanyika siku chache tu baada ya Sitta mwenyewe kuhojiwa na akaeleza kuzipuuza tuhuma dhidi yake, na akasema hakuwa tayari kuzitolea ufafanuzi kwa madai kuwa zilikuwa zikitolewa na wahuni.

Mbali ya hilo, Sitta alilielekeza Tanzania Daima kuwasiliana na maofisa wa Bunge ili kupata ukweli wote kuhusu madai hayo yaliyoandikwa katika mtandao mmoja wa intaneti.


 


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents