Habari

Mahakama yampa onyo Mtikila

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilitoa onyo kali kwa Mchungaji Christopher Mtikila, kutokana na kuidharau mahakama hiyo baada ya kutotokea katika siku ambayo kesi yake ilipangwa kusikilizwa.

na Asha Bani


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilitoa onyo kali kwa Mchungaji Christopher Mtikila, kutokana na kuidharau mahakama hiyo baada ya kutotokea katika siku ambayo kesi yake ilipangwa kusikilizwa.


Mchungaji huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), alitakiwa kufika mahakamani hapo Mei 16 mwaka huu, kusikiliza kesi anayoshitakiwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.


Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Khadija Msongo, Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi, Dustan Kombe, alimuomba hakimu kutoa onyo kali kwa mshitakiwa kutokana na kutohudhuria katika kesi inayomkabili siku ya Mei 16 ilipotajwa.


Mwendesha Mashitaka Kombe alimweleza hakimu kuwa, alipanga kwenda kumkamata Mtikila na kumwomba hakimu amfutie dhamana, kutokana na kutofika siku ya kesi hiyo, lakini kabla hajafanya hivyo Mtikila alijisalimisha mwenyewe mahakamani hapo jana.


“Endapo hatafika mahakamani tena bila ya kutoa sababu na kutoa taarifa, afutiwe dhamana na kurundikwa ndani,” Kombe aliiomba mahakama.


Mchungaji Mtikila alijitetea kwa kusema kuwa siku kesi hiyo ilipopangwa kutajwa, alikuwapo lakini kutokana na kutozoea utaratibu wa mahakama hiyo, alikaa nje kwa muda mrefu na kuamua kwenda Mahakama Kuu.


Alidai kuwa baada ya kwenda Mahakama Kuu alifuatwa na msaidizi wake na kumwambia kuwa alikuwa amekosea tarehe ya kesi ilikuwa si siku hiyo na yeye kuamua kuondoka.


Baada ya madai hayo, Mchungaji Mtikila alimtupia lawama msaidizi wake kwa kukosea kusoma diary yake inayomuongoza katika kesi.


Hakimu Msongo, alimpa onyo na kumwambia kama ana matatizo ambayo yatamsababisha kutofika mahakamani, anatakiwa kutoa taarifa kupitia mdhamini wake, na kuwa sababu alizotoa hazitoshelezi.


Katika kesi hiyo, Mtikila anakabiliwa na shitaka la kumkashifu Mkapa kwa kumtolea maneno ya kashfa wakati wa kipindi cha kampeni Julai 27, 2002 katika viwanja vya Jangwani.


Inadaiwa kuwa katika mkutano huo, Mtikila alitamka kuwa Mkapa si Mtanzania, ni raia wa Msumbiji.


Pia Mwendesha Mashitaka Kombe alidai kuwa, mbali na kumdhalilisha kwa kumwita si raia wa Tanzania, Mtikila alizidi kusema kuwa Rais Mkapa hana huruma na nchi ndiyo maana amediriki hata kusafirisha kontena la michanga ya dhahabu nje ya nchi.


Mbali na kumkashifu Mkapa, anadaiwa kumtolea maneno hayo aliyekuwa Waziri Mkuu katika serikali hiyo, Frederick Sumaye, kuwa ni gabachori, na ndiyo maana hana uchungu pia na nchi yake kama ilivyokuwa kwa rais huyo.


Hakimu Msongo aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 26 mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents