Majambazi watumia mabomu kupora abiria

Kundi la watu wasiozidi 15 wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za kivita, wamevamia basi moja la abiria kulilipua kwa mabomu na na kusababisha vifo vya watu wawili papo hapo

Kundi la watu wasiozidi 15 wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za kivita, wamevamia basi moja la abiria kulilipua kwa mabomu na na kusababisha vifo vya watu wawili papo hapo.

 

Tukio hilo ambalo ni la ajabu kutokea hapa kwetu Bongo, limetokea huko mkoani Kagera na kuzua hofu kubwa kwa wananchi waishio mkoani humo kwani katika historia ni nadra sana kwa hapa nchini kusikia wizi unaohusisha mabomu.

 

Akizungumza kwa njia ya simu leo asubuhi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Abdallah Msika amesema tukio hilo lilitokea jana saa 8:30 mchana katika pori la Kimisi lililo kati ya wilaya ya Karagwe na Ngara, wakati basi hilo lenye namba za usajili T 915 ANA aina ya Hino lililokuwa likitokea wilayani Karagwe kwenda Ngara, lilikuwa na abiria kati ya 30 na 35 huku likiendeshwa na Bw. Mwesiga Joseph.

 

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Msika amesema basi hilo lilipofika kwenye pori la Kimisi kwenye kona iitwayo Mnyonge ndipo walipojitokeza majambazi hao na kuanza kulishambulia kwa risasi, lakini askari wawili ambao walikuwa wakilisindikiza basi hilo, waliamua kujibu mashambulizi na kusimama kidete kutetea kazi yao.

 

Mapambano ya kurushiana risasi baina ya majambazi na askari hao, yalikuwa makali na majambazi yalipoona yamezidiwa nguvu, ndipo yakabadili silaha na kurusha mabomu ya mkono, baada ya hapo majambazi yaliwazidi nguvu Polisi na kufanikiwa kuingia ndani ya basi hilo na kuanza kupora mali za abiria.

 

Amesema yalipoingia ndani ya basi, yalimuona askari mmoja aliyekuwa amevalia sare, yakampiga risasi na kumuua papo hapo.

 

Kamanda Msika amemtaja askari huyo kuwa ni mwenye namba
MG 413657 Obadia Didas aliyekuwa akitokea Karagwe kwenda Benako.

 

Aidha Kamanda Msika amesema katika sakata hilo, majambazi hayo pia yalimpiga risasi na kumuua papo hapo mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa kari ya miaka 30 na 35.

 
Amesema askari huyo pamoja na majeruhi wengine wamelazwa katika Hospitali ya Mrugwanza mjini Ngara.

 

Kwa mujibu wa Kamanda Msika tayari polisi wameanza msako mkali katika pori hilo la Kimisi, ambapo tayari bunduki moja aina ya gobore imeshakamatwa na maganda 31 ya risasi za bunduki aina ya SMG na mabaki ya mabomu yameokotwa eneo la tukio.

 

Kamanda Msika amesema vikundi mbalimbali vya askari Polisi vimetumwa kuendesha msako katika pori hilo la Kimisi ili kukomesha vitendo hivyo vya uvamizi wa magari ambavyo vilikuwa vimeanza kutoweka.

 

Aidha Kamanda Msika amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa askari ili kufanikisha kuwakamata majambazi hao ambao katika uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa walikuwa wakizungumza lugha za Kirundi na Kinyarwanda.

 

Akasema pia uchunguzi huo wa awali umeonyesha kuwa miongoni mwa majambazi hao alikuwemo mwanamke mmoja.

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents