Tupo Nawe

Mambo 9 yaliyotawala muziki wa Bongo Flava mwaka 2016

Mwaka 2016 upo ukingoni kumalizika. Umekuwa ni mwaka mwingine wenye mafanikio makubwa katika tasnia ya muziki wa Tanzania. Japo kuna mambo mengi unayoweza kuwa nao kichwani pia, haya ni mambo 9 yaliyotawala zaidi muziki wa Bongo Flava mwaka huu:

1. Uhasama wa Team Kiba vs Team Diamond

Kadri siku zinavyoenda, ndivyo ambayo ushindani kati ya mashabiki wa Alikiba na Diamond unazidi kuwa mkubwa. 2016, ni mwaka mwingine ambao tumeshuhudia timu hizi zikisuguana kwa jazba, hasira, matusi, kejeli, vijembe na vurugu za maneno za kila aina ambazo wasanii hawa wamelazimika kuvumilia. Uhasama huu umeendelea kuwa mkubwa wa aina yake na uwanja mahsusi unaotumika kuuendeleza ni kwenye mitandao ya kijamii.

Shinikizo la mashabiki wao, limewafanya Diamond na Alikiba wafanye kazi kwa kujituma, kufikiria nje ya boksi na kwa umakini mkubwa ili tu kutowaangusha mashabiki wao, ama kutoa mwanya wa kukoselewa na timu pinzani. Ni wazi kuwa wakati mwingine, pressure hii ya mashabiki imekuwa ikiwalazimu wasanii hawa kufanya mambo ambayo hawakutarajia. Ni mchezo wa timing, ukizubaa unaachwa feli na mashabiki watakupongeza ukifanya vizuri lakini pia watakusulubu ukizingua.

Yahitaji akili za ziada kuushinda mtihani huu usio na kikomo, na kama Ali na Naseeb wangekuwa na roho nyepesi, wangeshindwa kustahimili, maake shughuli ni nzito. Katika timu hizi, kizuri mmoja anachokifanya ni kizuri kwa timu yake tu, lakini ni kibaya, upuuzi, pumba kwa timu nyingine.

Kasumba hii ilisababisha mjadala mkubwa kwenye tuzo za MTV MAMA mwaka huu baada ya Tanzania kuambulia patupu, na timu zikalaumiwa kuwa ni chanzo. Sisi kwenye habari, tunajua undani wa hisia zinazohusiana na kila kitu kinachomhusisha mmoja kati ya mafahari hawa wawili. Habari nzuri ya Diamond, ni mbaya kwa mashabiki wa Alikiba na watajitahidi kwa kila njia kuonesha kuwa hawajali, hata kama ni mafanikio kwa taifa zima. Vivyo hivyo, habari njema ya Alikiba, ni upuuzi tu kwa mashabiki wa Diamond, na wao pia watalipiza kisasi kwa kuiponda na kuikebehi kwa kila maneno ya shombo. Ndio mchezo ulivyo sasa, na wakati mwingine hauhitaji hasira.

Uhasama huu kiukweli hauoneshi kuisha leo wala kesho. Huu utaendelea kuwepo kwa kadri wawili hawa watakavyoendelea kufanya muziki. Na kwa kiasi kikubwa, licha ya matokeo hasi yatokanayo na vurugu na rabsha za timu hizi, uhasama huu umekuwa sehemu ya chanzo cha tasnia ya muziki ya Tanzania kuonekana ni wenye nguvu na macho ya Afrika kuimulika zaidi. Kwa mtu anayefahamu muziki, atakuambia kuwa uhasama huu ni wa muhimu kuchangamsha industry, ila cha kuzingatia tu usiwe na madhara yanayoweza kuhatarisha ustawi ama uhai wa wasanii hawa pendwa.

2. Ndoa za Mastaa

Katika kitu chanya ambacho wengi hawatokisahau mwaka huu, ni wasanii wengi kuuaga ukapela. Umekuwa ni mwaka wenye baraka nyingi zilizoifunua mioyo ya mastaa wengi walioamua kukamilisha moja ya hatua muhimu katika maisha ya binadamu – kuoa au kuolewa. Pamoja na hivyo, idadi kubwa hapa ni ya wanaume walioamua kuwaoa wachumba zao, huku kukiwa na idadi ndogo ya wanawake mastaa walioolewa.

Pamoja na hivyo, mastaa hawa wamekuwa mifano bora kwa wengine, na kujaribu kuondoa ile hofu kuwa ndoa kwa msanii ni kama big G na karanga – kwamba haviendi pamoja. Miongoni mwa wanamuziki waliofunga ndoa mwaka huu ni pamoja na: Mr Blue, Mwana FA, Luteni Karama, Tundaman, Manecky, Mabeste, Leo Mystereo (mume wa Riyamah) na Malick Bandawe aka Chiwa Man. Walioolewa ni pamoja na Kadjanito, Meninah na Kleyah.

3. Mwamko wa wasanii kuingia kwenye siasa

Mwaka huu Bongo Flava ilifanikiwa kuingiza mbunge mwingine mjengoni, Joseph Haule aka Profesa Jay, aliyechaguliwa kuwa mbunge wa Mikumi kupitia tiketi ya CHADEMA. Lakini pia Babalevo alifanikiwa kuchaguliwa kuwa diwani huko kwa Kigoma. Bahati haikuwaendea waimbaji wengine waliotupa karata zao wakiwemo Afande Sele, Kalapina, Keisha na wengine. Pamoja na waimbaji, waigizaji nao walijitokeza kujaribu bahati zao wakiwemo Wema Sepetu na Irene Uwoya.

4. Video bora zaidi za muziki

Katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania kwa sasa inaongoza kwa kuwa na video nyingi zenye ubora na zinazojulikana. Mwaka 2016, umeshuhudia wasanii wengi wakiingia zaidi mifukoni mwao kufanya video zenye ubora na huku wakiwatumia waongozaji mahiri. Wasanii kama Mwana FA, Fid Q, Ben Pol, Belle 9 na wengine, mwaka huu waliongezeka kwenye orodha ya wasanii wa Bongo waliosafiri hadi Afrika Kusini kwenda kufanya video zenye viwango vikubwa. Na hakika wengi uamuzi huu umewaletea matunda sababu video hizi zimewasaidia kuyafikia matawi ambayo hawakuwahi kuyafikia.

5. Views za Youtube

Tanzania ni moja ya nchi ambazo gharama za internet ziko chini sana Afrika. Na kwakweli, licha ya mapenzi makubwa kwa wasanii wetu, hiyo ni sababu kubwa kwanini video za wasanii wa Tanzania zinapata views nyingi kwenye mtandao wa Youtube. Mwaka 2016, hata hivyo ulikuwa na utofauti mkubwa. Tumeshuhudia wasanii wengine wakifikisha views milioni 1, kitu ambacho miaka miwili iliyopita kilikuwa kikifikiwa na wasanii wachache tu, hasa Diamond na Alikiba.

Mwaka huu wasanii kama Mwana FA, Darassa, Ben Pol, Mr Blue, Jux, Vanessa Mdee na wengine nao wamefurahia idadi kubwa ya views mwaka huu. Lakini katika kuonesha kuwa wasanii wetu wana watazamaji wengi nje ya nchi pia, takwimu za Google mwaka huu zimeonesha kuwa Salome ya Diamond ndio video ya muziki iliyoangaliwa zaidi kwenye Youtube nchini Kenya.

6. Rap yapiga hatua

Jitihada za wasanii wa rap kwenda sambamba na waimbaji hazijaanza mwaka huu pekee. Ukimtoa AY ambaye kwa ujumla ndiye muasisi wa kuvuka boda na kwenda kushoot video kali, kipindi cha miaka miwili iliyopita, Joh Makini amekuwa mstari wa mbele katika kuwekeza fedha nyingi katika video zake. Lakini mwaka huu, wasanii wengi zaidi wa rap wameamka. Uamkaji huo ni sababu ya kuibuka kwa hits za wasanii wa rap zinazofanya vizuri sambamba na hits za waimbaji ama zaidi. Mfano halisi wa mafanikio ya rap mwaka huu ni Darassa ambaye amefanikiwa kuachia ngoma tatu zilizohit kwa kuongoza – Kama Utanipenda, Too Much na sasa Muziki.

Muziki imevunja rekodi nyingi zake mwenyewe na za ujumla. Ndio wimbo namba moja kwa sasa Tanzania na huku ukifanya vizuri nje ya nchi hadi kushika namba 1 kwenye chati za Afrika za Trace TV. Lakini pia ikiwa na mwezi mmoja na wiki moja, Muziki imeweza kuvutia views zaidi ya milioni 2.5 kwenye mtandao wa Youtube, rekodi ambayo iliweza kufikiwa na AY kwenye Zigo Remix aliyomshirikisha Diamond.

Nyimbo kama Asanteni kwa Kuja na Dume Suruali za Mwana FA, Chafu Pozi ya Bill Nas, Mboga Saba ya Mr Blue f/ Alikiba, Pesa ya Madafu ya Jay Moe, Roho ya Fid Q f/ Christian Bella, Perfect Combo ya Joh Makini f/ Chidinma , zimekula sahani moja na hits za waimbaji.

7. Singeli kuingia mainstream

Mwaka huu Singeli imezalisha majina makubwa ya wasanii kama Man Fongo, Sholo Mwamba na wengine. Muziki huo uliokuwa maarufu kwenye sherehe za uswahilini na vichochoroni jijini Dar es Salaam na kutafsiriwa kama wa wahuni na wavuta bangi, umefanikiwa kuingia mainstream na redio kuzicheza kama nyimbo zingine. Mwaka 2016, kituo cha redio cha EFM, kitakumbukwa kwa mchango kwenye kusaidia kueleweka kwa muziki huu kupitia jitihada zake za kuucheza kwa wingi. Baada ya muda redio zingine nazo zikaanza kucheza baadhi ya nyimbo za wasanii wa Singeli ambao walianza kupata nafasi za kutumbuiza kwenye majukwaa ya kawaida na kulipwa fedha kama walipwavyo wasanii wa Bongo Flava.

Lakini pia nguvu ya muziki wa Singeli uliweza kuwavutia wana hip hop wakiwemo Profesa Jay, Roma na Baghdad pamoja na msanii wa R&B, Rama Dee kuweka vionjo vyake kwenye nyimbo zao.

“Nimefanya hip hop singeli kwaajili ya kuupeleka muziki huo mbali lakini pia kuitengeneza hip hop tofauti,” alisema Profesa. “Kuliko kuwakopi akina Lil Wayne wanafanyaje basi tufanye muziki ambao tutakopi muziki wa nyumbani. Nadhani ni muda sasa hivi wasanii wa hip hop kutanua, wasikopi vya Marekani, wako vya Tanzania ili kuifanya hip hop yetu ibadilike kila siku,” aliongeza.

Na hata Vanessa Mdee alisema Singeli ni muziki wa aina yake.
Vanessa pia anautabiria makubwa muziki huo. “The drum percussion is so unique,” alikiambia kipindi cha 5 Select cha EATV miezi kadhaa iliyopita. Vee Money aliongeza kuwa maproducer wakubwa kama Major Lazer na Pharrell Williams wamekuwa wakiufuatilia muziki wa Afrika kwa ukaribu na huenda masikio yao yakaja kutua kwenye muziki wa Singeli.

Belle 9 na Juma Nature kwa upande wao walikuwa na mtazamo tofauti.

“Sitegemei kufanya Singeli,” alisema Belle. “Hata kama nitafanya, sitofanya kama release song sababu Singeli ni muziki fulani hivi ambao unapita, ni bubble gum music. Sasa hivi watu wanaushabikia lakini itafika time utapita, sio muziki wa kustick.”

Naye Nature alisema, “”Singeli itapita tu kwasababu ya uhuni,” aliambia Bongo5. “Unajua raia wengi wa Bongo hawapendi mambo ya kipumb*vu pumb*vu na mashabiki wetu wengi sana sio wahuni ila wahuni wanakuja katika hizi section, so wakija kwenye section hapo muziki hakuna tena,” aliongeza.

Swali ni je? Muziki huo utaendelea kufanya vizuri mwaka 2017?

8. Kuibuka kwa label za muziki

Mwaka huu tumekuwa na mfano hai wa label ya muziki ya wazawa inayoweza kuwakuza wasanii wakawa wakubwa kiasi cha kujulikana Afrika nzima. Label ya Diamond, WCB, ni mfano hai wa label ya muziki iliyofanikiwa Afrika Mashariki. Ikiwa ni nyumbani kwa wasanii wanaotikisa kwa sasa, Ray Vanny, Rich Mavoko, Harmonize, Queen Darleen na CEO mwenyewe, Diamond, WCB imegeuka kuwa kisima cha hits barani Afrika. Pamoja na WCB, mwaka huu zimeanzishwa label zinazofanya vizuri ikiwemo The Industry ya Navy Kenzo, PKP ya Ommy Dimpoz, High Table Sound ya Barnaba, na zingine lukuki ambazo zinajikongoja. Lakini pia wasanii kama Dully Sykes, Ray Vanny na wengine wameonesha nia ya kuanzisha zao.

9. Ushindani kwenye vituo vya redio

Mwaka 2016 hautosahaulika kwa ushindani mkubwa uliokuwepo kwenye vituo vya redio. Ushindani mkubwa ulioshuhudiwa ulikuwa ni kati ya EFM na Clouds FM zilizochukuliana watangazaji back to back. Miongoni mwa ukwapuaji uliotia fora ni wa Gardiner G Habash kutoka EFM kurudi Clouds FM, Paul James na Gerald Hando kutoka Clouds kwenda EFM na kisha PJ kurejea tena Clouds. Mwingine ni Clouds kumkwapua Kicheko kutoka EFM. Lakini pia East Africa Radio nayo iliumizwa baada ya kuchukuliwa kwa watangazaji wake Mamy Baby na DJ Sinyorita.

Mwaka 2017, bila shaka utakuwa na mambo makubwa zaidi..

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW