Mauaji Afrika Kusini: Watanzania wakimbilia polisi

Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini, wamekimbilia kituo cha polisi cha Jeppe, jijini Johannesburg na sasa wameiomba serikali ya Tanzania iwasaidie waweze kurejea nchini.

Na Sammy Kassika, PST Sumbawanga

Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini, wamekimbilia kituo cha polisi cha Jeppe, jijini Johannesburg na sasa wameiomba serikali ya Tanzania iwasaidie waweze kurejea nchini.

Watanzania hao walitoa ombi hilo wakati wakizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana kufuatia serikali za Malawi, Msumbiji, Zimbabwe, Lesotho, Botswana na Ethiopia, kuamua kuwarejesha nyumbani raia wao.

Walilazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na mauaji dhidi ya raia wa kigeni yanayoendelea nchini Afrika Kusini.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mtanzania huyo Bw. Seleman Hassan (33), alisema wamekimbilia katika kituo hicho kuanzia mapema wiki hii wakihofia usalama wao na kwamba hawana kitu chochote.

Alisema licha ya kuporwa mali walizokuwa nazo, baadhi yao wamejeruhiwa na wapo kituoni hapo wakiwa hawana msaada wowote.

Walisema tangu wajisalimishe kituoni hapo, juzi walipata fursa ya kuzungumza na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini humo, Bw. Felix Mwijarubi.

Bw. Hassan ambaye makazi yake kwa hapa nyumbani alisema ni Kunduchi Mtongani, jijini Dar es Salaam alisema anaomba msaada ili yeye pamoja na wenzake, waweze kurejea salama.

Alidai kuwa, serikali ya Afrika ya Kusini ina mpango wa kuwajengea mahema ili waweze kuishi kama wakimbizi hadi hapo watakapoweza kupata nauli ya kurejea nyumbani.

Hata hivyo, alisema mpango huo utakuwa mgumu kwao kwa vile hawana kitu chochote baada ya kuporwa kila kitu walichokuwanacho na wakazi wa huko ambao wamejenga chuki dhidi ya wageni wakidai kuwa wamechukua nafasi zao za ajira.

Bw. Hassan alisema anafanyakazi katika kampuni ya kusambaza madawa.

Kwa upande wake, Bw. Ramadhan Athuman (32) ambaye hufanya biashara mbalimbali alisema kuwa amechomwa kisu kifuani katika vurugu hizo.

Alisema hana hamu ya kuendelea kuishi nchini humo na anapenda kurudi nyumbani lakini kwa sasa hana nauli.

Wakizungumzia kuhusu uwezekano wa baadhi ya Watanzania kufa, Bw. Hassan alisema inawezekana kwa kuwa wapo wengi na hawafahamiani.

Alisema inawezekana baadhi wakawa wameuawa kwa kuwa wengi wao wanaishi kwa kudanganya uraia.

Alisema katika mazingira kama hayo, sio rahisi kujua Watanzania waliopoteza maisha.

Juhudi za kumpata Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe ili azungumzia suala hilo zinaendelea.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents