Mauritius kusaidia ulinzi teknolojia Tz
SERIKALI ya Mauritius imeonyesha nia ya kuisaidia Tanzania katika kuimarisha ulinzi wa Teknolojia ya habari na Mawasiliano (Teknohama) ambapo pamoja na mambo mengine, utaalamu huo utaliwezesha Taifa kupiga hatua kubwa katika upande huo.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Makame Mbarawa, mara baada ya ziara yake katika Taasisi ya teknolojia ya Dar es salaam (DIT) akiambatana na Waziri wa Elimu, Sayansi na utafiti wa teknolojia wa Mauritius Dkt. Rajesh Jeetah.
Mbarawa alisema wakati huu ambapo Tanzania inazidi kujiimarisha katika nyanja ya teknolojia, Serikali ya Mauritius tayari ilishafanikiwa katika suala hilo hivyo ushirikiano wa kimawasiliano ambao Mataifa yote mawili yameuonyesha, utalisaidia Taifa letu kufikia kiwango kizuri.
Aidha amewataka wataalamu wa masuala mbalimbali kutojificha badala yake wajitokeze kwa wananchi ili waweze kuwasaidia katika masuala waliyobobea ambapo kwa kufanya hivyo alisema kutasidia kuondoa mapungufu wa wataalamu, kama hali ilivyo sasa.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na utafiti wa teknolojia wa Mauritius Dkt. Rajesh Jeetah, alisema nchi yake kwa sasa imejidhatiti katika masuala mbalimbali ya teknolojia zikiwemo za mawasiliano na uendeshaji wa mitambo, hivyo inataka ibadilishane utalaamu ilionao na Tanzania.
Alisema kwa kuanza Serikali yake imechukua jukumu la kuwafundisha watalaam saba ambao mara baada ya mafunzo hayo watakayoyapewa wataweza kushirikiana na wataalamu wengine waliopo nchini katika nyanja nzima ya teknohama.