Habari

Mganga Mkuu ‘amtilia ngumu’ Mbunge

MBUNGE wa Viti Maalumu mkoa wa Shinyanga, Bi Mercy Emmanuel (CUF) amedai kudhalilishwa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa, Dkt. Amos Mlemi alipokwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu.

Na Samwel MWanga, Maswa

 

MBUNGE wa Viti Maalumu mkoa wa Shinyanga, Bi Mercy Emmanuel (CUF) amedai kudhalilishwa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa, Dkt. Amos Mlemi alipokwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, mbunge huyo alidai kuwa alifika hospitalini jana saa 1.30 asubuhi kupata matibabu na ushauri zaidi kutoka kwa mganga huyo, kwani hali yake ya kuvimba mkono ilikuwa inazidi kuwa mbaya.

 

Alidai kuwa alishapata matibabu ya awali kwa muda wa siku saba katika hospitali hiyo, baada ya mkono wake wa kushoto kuvimba kiganja, lakini hali iliendelea kuwa mbaya, hivyo kuamua kumwona Mganga Mkuu kwa matibabu na ushauri zaidi.

 

Alidai kuwa alipofika alifuata taratibu zinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kusajiriwa na kupatiwa cheti namba 5726/08 na kuelekezwa zilipo ofisi za mganga huyo.

 

Mbunge huyo alizidi kudai kuwa alipofika ndani ya ofisi ya mganga huyo alimweleza kuwa hana muda wa kumsikiliza kwa sasa kwani anawahi kikao cha asubuhi hivyo asingeweza kusikiliza mgonjwa yeyote.

 

Alidai licha ya kumsihi na kumweleza kuwa anajisikia maumivu makali hivyo amsikilize, lakini mganga huyo alimtolea maneno makali na kumweleza kuwa ni lazima ahudhurie kikao na baadaye atasikiliza na kutibu wagonjwa na kumwamuru atoke ofisini mwake mara moja.

 

Alizidi kudai kuwa mganga huyo alimweleza kuwa kama hataki kufuata utaratibu huo ambao amemweleza basi aondoke akatafute matibabu sehemu nyingine, hali aliyodai ilimdhalilisha mbele ya wagonjwa wengine na kwa baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo waliokuwa katika eneo la tukio.

 

Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo walimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa kitendo alichokifanya mganga huyo ni kinyume na utaratibu ni vizuri angemsikiliza mteja wake ambaye alifika ofisini kwake lakini hata hivyo hakutaka kujitambulisha kwani alifika kupata huduma ya matibabu kama Mtanzania mwingine.

 

Baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo walidai kitendo cha Dkt. Mlemi dhidi ya mbunge huyo ni mwendelezo wa kauli ambazo amekuwa akizitoa kwa watumishi wa hospitali hiyo tangu alipohamishiwa hapo hivi karibuni kutoka hospitali ya wilaya ya Iramba, Singida.

 

Naye Mganga huyo alipoulizwa kuhusiana na malalamiko hayo, alidai kuwa alimweleza mbunge huyo amsubiri ahudhurie kikao hicho ndipo aweze kumsikiliza.

 

“Mimi nilimweleza anisubiri, lakini yeye ilionekana kwamba hataki… kwa hali hiyo siwezi kufanya kazi na kwa sasa naiomba wizara iniondoe siwezi kuendeshwa na wanasiasa,” alisema Dkt. Mlemi.

 

Mkuu wa Wilaya hiyo, Kapteni mstaafu, James Yamungu alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa mbunge huyo na kudai kuwa suala hilo kwa sasa analishughulikia na kuwa si kubwa sana kama mbunge huyo anavyofikiria.

 

“Nafikiri daktari hakuwa na nia mbaya, lakini jambo hili mnataka kulikuza kwani nimeonana na daktari mwenyewe, nafikiri mheshimiwa mbunge alipoelezwa kusubiri akaona amedhalilishwa, mimi nakusihi jambo hili mlione kama la kawaida,” alisema Kapteni Yamungu.

 

 

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents